Vitendo vya kigaidi venye asili ya uchochezi wa kidini, kinzani za kisiasa, kijamii
na kikabila ni kati ya mambo ambayo yameendelea kuchangia kuporomoka kwa misingi ya
haki na amani sehemu mbali mbali za dunia. Hakuna sababu za msingi zinazoweza kuhalalisha
vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa amani na kwamba, mwanadamu kimsingi ni mtu mwenye
imani na wala hakuna utamaduni usiojengeka katika msingi wa imani.
Uhuru wa
kidini ni msingi wa haki nyingine zote za mwanadamu, unaoonesha uhusiano kati ya mwanadamu
na Muumba wake na kati ya wanadamu wenyewe. Ni wajibu wa Serikali husika kuhakikisha
kwamba, inatoa haki sawa kwa raia wake katika masuala ya uhuru wa kidini, kama sehemu
ya mchakato wa kulinda na kudumisha mafao ya wengi. Demokrasia ya kweli inawajibu
wa kuthamini uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na ule wa mwamini kutoa mawazo na maoni
yake.
Haya ni baadhi ya mawazo msingi yaliyotolewa na Kardinali Jean Louis
Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wakati alipokuwa anashiriki
kwenye mkutano wa urafiki miongoni mwa watu wa Mataifa mjini Rimini, nchini Italia.
Uhuru wa kidini unagusa dhamiri ya mtu, mahali patakatifu panapomwezesha mtu kutambua
jema la kufuata na baya la kuepuka. Uhuru wa kidini ni sehemu ya vinasaba vya ukweli
na wala si jambo la shuruti kutoka nje.
Imani ni jambo shirikishi linalowajumuisha
watu wanaoamua kufuata: Ibada, Imani na Mafundisho pamoja na kujenga uhusiano wa dhati
na Mwenyezi Mungu, jambo la hali ya juu kabisa ambalo mwanadamu anaweza kulitenda
bila kizuizi kutoka nje. Dini inaonesha uhusiano wa mwanadamu na Mwenyezi Mungu; kiumbe
na Muumba wake. Madhehebu mara nyingi yanaonesha ili hali ya binadamu kutaka kutawala
nguvu za Kimungu kwa ajili ya mafao yake binadamu.
Kardinali Tauran anasema
kuna haja kwa Serikali na dini mbali mbali kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya wengi na kwamba, waamini wa dini mbali mbali duniani wanalo jukumu la kuchangia
maendeleo ya nchi zao. Waamini ni rasilimali watu inayoweza kutumika kwa ajili ya
mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya
kiroho, kiutu na kimaadili. Waamini wapewe nafasi ya kushiriki katika Ibada; wawe
na uhuru wa kushirikiana na watu wengine imani yao na kwamba, kwa pamoja waamini wana
dhamana ya kulinda na kudumisha amani.
Kardinali Tauran anabainisha kwamba,
imani ni nguvu msingi katika ujenzi wa amani. Kwani hapa utu na heshima ya binadamu
inapewa kipaumbele cha kwanza; daima waamini wakichangamotishwa kusimama kidete kutafuta
mafao ya wengi; wakielimishana katika ukweli na uwazi; maadili na utu wema ili kujenga
Jamii inayosimikwa katika udugu, upendo na mshikamano wa kweli.
Tofauti za
kiimani kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu na kinzani za kijamii, bali kikolezo cha
mshikamano wa dhati. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuwa ni mfano na ushuhuda
wa misingi ya maadili na utu wema. Dini ikiondolewa katika maisha ya mwanadamu, hapo
patakuwa ni patashika nguo kuchanika!