2013-08-23 08:28:44

Rais Kikwete na changamoto za elimu nchini Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameyapatia ufumbuzi matatizo makubwa na ya muda mrefu ambayo yamekuwa yanawakabili wahadhiri na wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini.

Katika kikao kilichofanyika Ikulu, Dar Es Salaam Jumatano, Agosti 21, 2013 kwa muda wa saa sita kati ya Rais na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Remmy Assey kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliamua na kuelekeza ifuatavyo:

(1) Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, ihakikishe kuwa Bajeti ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma ambayo imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka inarejeshwa kwenye viwango vya zamani mapema iwezekanavyo, na kwamba bajeti hiyo isiwe inapungua mwaka hadi mwaka kama ilivyo sasa.

(2) Nyongeza ya fedha hizo itumike kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma. Shughuli hiyo ianze kwa kufanyika tathmini ya kujua vipaumbele, na kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji.

(3) Madai ya wanataaluma yatokanayo na stahili zao, na ambayo yamehakikiwa yalipwe kwa awamu na kazi ya uhakiki wa madeni mengine iendelee.

(4) Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ishirikiane na Viongozi wa Vyuo hivyo kupitia upya Muundo wa Utumishi (Scheme of Service) kwa ajili ya wanataaluma kwa lengo la kuuboresha kwa kuzingatia mahitaji maalum ya wanataaluma.


(5) Vyuo Vikuu vya Umma virejeshewe uhuru wa kuajiri wanataaluma moja kwa moja bila ya shughuli hiyo kufanywa na Sekretarieti ya Ajira Serikalini.

(6) Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikutane na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma haraka iwezekanavyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya upandishaji vyeo wanataaluma na nyongeza za mishahara za kila mwaka.

(7) Utaratibu wa Mikopo ya Ujenzi wa Nyumba kwa ajili ya Watumishi wa Serikali ulioanzishwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhusishe pia Wanataaluma wa Vyuo Vikuu. Aidha, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vyenye ardhi ya kujenga nyumba za kuishi wanataaluma vijadiliane na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye wanachama kwenye vyuo hivyo ili kuona uwezekano wa Mifuko hiyo kujenga nyumba za kuishi za wanataaluma kwenye maeneo hayo.

(8) Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mdhibiti wa Mifuko hiyo washirikiane haraka na Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma pamoja na Serikali ili kulipatia ufumbuzi tatizo la uwasilishaji wa michango ya pensheni ya wanataaluma.

Rais na viongozi wa wanataaluma hao wamekubaliana kukutana tena baada ya miezi mitatu kupokea taaarifa ya utekelezaji na kufanya maamuzi kuhusu maeneo mengine yanayoendelea kuchambuliwa kwa kushirikiana kati ya Serikali, Uongozi wa Vyuo na Uongozi wa Muungano wa Wanataaluma.

Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini walimshukuru Rais kwa hatua hizi na maamuzi yake katika kushughulikia matatizo yao ya siku nyingi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyobaki.








All the contents on this site are copyrighted ©.