2013-08-23 12:24:13

Mabruda wa FIAT Dodoma wanaadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu kuanzishwa!


Shirika la Mabruda wa Fiat, Jimbo Katoliki Dodoma ni matunda ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Hili ni Shirika la Kitawa lenye hadhi ya Kijimbo ambalo katika kipindi cha miaka 25 limepitia changamoto mbali mbali, lakini bado linasonga mbele kwa imani na matumaini, huku likishiriki maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Dodoma.

Ni ushuhuda wa Askofu mstaafu Mathias Josefu Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Shirika la Mabruda wa FIAT, Jimbo Katoliki Dodoma lilipoanzishwa hapo tarehe 15 Agosti 1988. Askofu mstaafu Isuja anasema, hii ilikuwa ni siku ya kufunga Mwaka wa Bikira Maria Mama wa Mkombozi uliotangazwa na kuzinduliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kwa kutoa heshima ya pekee kwa Bikira Maria, kioo na kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza, jambo linalojionesha kwa namna ya pekee katika Jibu lake la "NDIYO", Yaani FIAT kwa lugha ya Kilatini.

Bikira Maria kupalizwa mbinguni anasema Askofu mstaafu Isuja anasema kwamba, ni kielelezo cha imani na matumaini ya Kanisa katika maisha ya uzima wa milele baada ya kukamilisha hija ya maisha ya hapa duniani, waamini wanatarajia kuungana na kuishi na Mwenyezi Mungu milele yote. Bikira Maria ni kielelezo cha ufuasi makini wa Kristo na utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika kazi ya ukombozi.

Bikira Maria ni tunda la kwanza la Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, ambayo Bikira Maria alishiriki kwa namna ya pekee katika hija ya maisha yake hapa duniani, tangu kutungwa mimba kwa Neno wa Mungu, hadi aliposimama chini ya Msalaba akapokea maiti ya Mwanaye Mpendwa. Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho ni upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwanaye Yesu Kristo.

Askofu mstaafu Isuja anasema, Mabruda wa FIAT Jimbo Katoliki Dodoma wanaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa kwa njia ya maisha ya: Sala, tafakari ya Neno la Mungu na Kazi. Hii ni changamoto kwa Mabruda hao kuendelea kuishi kadiri ya taratibu na kanuni za maisha ya kitawa mintarafu sheria za Kanisa, Miongozo ya Kanisa na Maaskofu.

Watawa wanapaswa kutambua kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia wanakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha yao, wasipokuwa makini, wanaweza kumezwa na malimwengu na huko watakiona chamtema kuni!







All the contents on this site are copyrighted ©.