2013-08-23 12:08:54

Jengeni utamaduni wa kutetea utu wa binadamu kwa kukazia upatanisho na mshikamano wa kitaifa


Kuna mamillioni ya watu ambao wamepoteza maisha kutokana na dhuluma na nyanyaso zilizofanywa na tawala za kidhalimu Barani Ulaya. Hawa ni wananchi waliokuwa wanatamani kuishi katika mazingira ya haki, amani, utulivu na maendeleo, lakini wakakumbana na ukatili ambao umeacha kurasa chungu katika maisha ya wananchi wengi Barani Ulaya.

Katika mazingira kama haya, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusimama kidete kulinda na kutetea: maisha, utu na heshima ya binadamu sanjari na kukazia upatanisho na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.

Ni changamoto iliyotolewa na Askofu mkuu Julius Janusz, Balozi wa Vatican nchini Slovenia katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya wahanga wa tawala za kimabavu Barani Ulaya. Katika mahubiri yake anasema, Kanisa linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema kwa njia ya Mafundisho Jamii, kusimama kidete kulinda na kutetea: uhai, uhuru na demokrasia ya kweli; utu na heshima ya binadamu pamoja na haki zake msingi.

Imani iwajengee waamini uwezo wa kusamehe na kuanza mchakato wa upatanisho, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji, Lumen Fidei, Mwanga wa Imani.

Waamini wawe ni vyombo vya ujenzi wa misingi ya haki, amani na upendo, kwa kujitahidi kumwilisha ndani mwao, ile Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani; wakitafuta, haki na amani na kwamba, nyanyaso na madhulumu ya kidini kwa msingi wa kundi fulani kutaka kujijenga kisiasa au kijamii ni jambo ambalo haliwezi kukubalika. Mwanga wa imani uwasaidie waamini na watu wenye mapenzi mema kutembea katika upendo, unaowasukuma kutafuta mafao ya wengi, kwa kukazia haki na amani.

Kurasa chungu za madhulumu na nyanyaso za utu na heshima ya binadamu, iwe ni fursa ya kuomba na kutoa msamaha ili kujenga utamaduni wa Upatanisho, Haki na Amani. Hii ndiyo changamoto inayoendelea kutolewa na Mama Kanisa wakati huu ambayo bado kuna vita, kinzani na migogoro ya kijamii na kisiasa; kwani Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira. Kumbu kumbu hii iwe ni nafasi ya kuendelea kuunga mkono juhudi za kuleta ukombozi kwa wale ambao bado wako kwenye kongwa la talawa dhalimu sehemu mbali mbali za dunia.All the contents on this site are copyrighted ©.