2013-08-23 08:39:22

Amri kuu ya upendo na changamoto zake!


Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote....
Tafakari ya Agosti, 23, Ijumaa:

Mwimbaji Cosmas Chidumule anatukumbusha njiwa katika viota vyao wanapendana, kumbi kumbi wapendanao wanaambatana wawili wawili kwa upendo katika kichuguu. Binadamu pia wana upendo huo huo baina ya wawili. Tarehe 14 Februari imeshika kasi kubwa kwa miaka hii kwa sikukuu ya wapendanao - Valentine Day. Katika upendo huu Wote wa wadudu, wanyama na binadamu ni upendo wa kawaida, au ni upendo wa daraja la chini. Upendo wa kimungu ni wa daraja la kwanza "Agape"

Leo Kristo anatuambia kuwa kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, kwa akili zetu zote - ni amri inayobeba torati yote. Ni kurudi katika mwito wa "Shema Israeli" (Kumb 6:4). Amri hii ni muktasari wa amri 613 zilizowasumbua daima Waisraeli kiasi ambacho katika maisha yote mtu alishindwa kukumbuka kwa uhakika ni amri ipi aliivunja au kaitekeleza vizuri.

Mwalimu mzuri wakati wa Yesu alikuwa ni yule aliyeweza kuziweka kwa ufupisho au muktasari sana amri hizi huku amesimamia mguu mmoja tu ! Yesu anataka kusema nini kwetu sisi leo na kwa Mafarisayo wa wakati ule
(Mt 22:34-40):

1. Kumpenda Mungu kunahitaji kwa nafasi ya kwanza kuwa uchaji na ibada mbele ya Mungu. Musa aliambiwa kila anapokutana na Mungu ahakikishe kuwa ana usafi wa moyo au kiroho ndani yake "vua viatu vyako" (Kutoka 3:5). Yaani, kuhakikisha kuwa tunapomwendea Mungu kwa ibada tusiwe na lawama na wenzetu au na Mungu mwenyewe (Zaburi 15:1 - 5). Ukipeleka sadaka yako kwa Bwana, patana na mshtaki wako kwanza (Mt 5:23). Upendo huu watuhitaji kuwa na utakatifu au ukamilifu kama Mungu wetu aliye mtakatifu (Mt 5:48).

Upendo wa binadamu uoneshwe kwa ibada zetu za kila mara kanisani. Tusiache tu ndege na shomoro wajenge viota katika madhabahu ya Bwana na sisi tumelala nyumbani (Zab 84:3). Kuna wenzetu ambao huliona Kanisa siku za mkesha wa Krismasi au Pasaka tu. Siku nyingine wanalala tu nyumbani. Watu wapo "busy" na biashara zao au kwenda City na mashambani siku za Dominika. Wanasahau "shika kitakatifu siku ya Bwana.."

2. Kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote kunahitaji tujipange kwa matoleo yetu kwake. Fedha dhahabu ni mali ya Bwana. Yesu anaisifu sadaka ya mjane inayotolewa kwa kipimo cha upendo mkubwa (Marko 12:41-44). Mjane hafikirii maisha yake, anampa Mungu nafasi ya kwanza. Nabii Malaki anakuwa mkali kwa kutukumbusha kuleta matoleo ya kutosha hekaluni kwa ajili ya shughuli za Kanisa na wahitaji - "Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha.. (Malaki 3:10)

3. Baada ya kumpenda yule Mungu mkuu kabisa tusiyemuona, Kristo anatualika kumpenda yule tumuonaye kila siku - jirani yetu. Kipimo cha upendo wa ndugu au jirani ni kama tunavyojipenda sisi wenyewe. Jirani yako wa kwanza ni mke na watoto wako. Mfano wa Msamaria Mwema (Luka 10:24 - 37) utupe swali hili, Je, hakuna watoto wanaolala bila chandarua, chakula kisichotosha, kitanda kibovu, wamefukuzwa shule kwa kutokuwa na karo - wakati baba anajenga jina kwa vimada ?

Hakuna mama anayeuza vitumbua na samaki wa kukaanga jioni wakati baba ana mshahara na marupurupu ya ukurugenzi wa wizara? Au, Je, hakuna mama anayevaa mikufu ya dhahabu ya gharama wakati mtoto wake akienda kliniki anakutwa na Kwashakoo ?

Tusali mioyo yetu iwe na upendo kwa Mungu. Tumpende kwa ibada safi za mara kwa mara. Tujiombee pia tuwe na upendo na jirani zetu wa kwanza - yaani, familia zetu kwa vile "charity starts at home"


Mtumishi wenu,Padre Beno Michael Kikudo
Jimbo kuu la Dar es Salaam.
All the contents on this site are copyrighted ©.