Ukosefu wa fursa za ajira unawatumbukiza wengi katika umaskini wa kipato!
Mtandao wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Uingereza, CSAN, limepokea
taarifa ya Serikali ya Uingereza kuhusu kupungua kwa ukosefu wa fursa za ajira nchini
humo, lakini umeiomba Serikali kuendelea kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba,
inajipanga barabara kukabiliana na tatizo la ukosefu wa fursa za ajira nchini Uingereza
kama sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato.
Katika
kipindi cha kuanzia mwezi Aprili 2013 hadi Mwezi Juni 2013, takwimu za kitaifa zinaonesha
kwamba, watu 4,000 walikosa fursa za ajira nchini Uingereza. Hali hii ina madhara
makubwa kwa wafanyakazi pamoja na familia zao wanaoendelea kukabiliana na hali ngumu
ya maisha kwani kuna baadhi ya familia zinashindwa kupata mahitaji yake msingi kutokana
na ukata wa maisha ambao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa.
Zaidi ya watu millioni tano wanapokea mshahara ambao hauwezi kukidhi
mahitaji msingi ya familia, hali ambayo inaendelea kuwatumbukiza watoto wengi nchini
Uingereza katika hali ya umaskini. Hii ni kashfa ya umaskini inayowaandama wafanyakazi
wanaoendelea kupokea mshahara usiokidhi mahitaji msingi ya wafanyakazi.
Mtandao
wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Uingereza unaendelea kuihamasisha
Serikali kuhakikisha kwamba, inatoa mishahara ya haki na mafao msingi kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wafanyakazi, kama sehemu ya mchakato unaopania kuleta mabadiliko
katika mfumo wa ajira unaozingatia haki.
Hii ni changamoto iliyotolewa na
Askofu mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, hivi karibuni
alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Mtandao wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki
nchini Uingereza.
Alisema, balaa la umaskini linaendelea kushika kasi ya ajabu
nchini Uingereza, kiasi kwamba, wafanyakazi wengi wanajikuta wanapokea mishahara ambayo
haikidhi gharama za maisha, kiasi cha kuwafanya kuwa ni tegemezi kwa Mabenki ya chakula
kwa ajili ya mikopo ya chakula kila mwezi. Hii ni changamoto kwa Serikali, Sekta binafsi
na Jamii kwa ujumla na kwa wote ambao wanapaswa kutoa maamuzi ya kina kwa ajili ya
wafanyakazi na familia zao.