Makatekista ni kati ya wadau wakuu wa azma ya Uinjilishaji ndani ya Kanisa kwani jukumu
lao kubwa ni kuwaandaa Wakatekumeni ili waweze kupokea vyema Sakramenti za Kanisa.
Makatekista wengi wamekuwa ni mfano na mwanga kwa Jumuiya inayowazunguka.
Kanisa
linaendelea kuwashukuru Makatekista kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa.
Hili ni kundi ambalo linahitaji kupatiwa majiundo ya kina na endelevu ili liweze kutekeleza
dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa. Lakini, wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa,
kwani mfanyakazi mwaminifu katika shamba la Bwana anastahili kupata ujira wake.
Makatekista
wanaendelea kuchangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa ushuhuda wa
imani tendaji kwa njia ya maisha na matendo yao adili, kwa kuwajali wote bila ubaguzi.
Ni mwaliko wa kumwilisha Injili na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, ili kutoa Katekesi
safi na kina kwa watu wao; wakiwaongoza kwa moyo wa Sala na Ibada. Kama sehemu ya
viongozi wa Kanisa wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ujasiri na bidii, ili kuchangia
utakatifu wa maisha ya Familia ya Mungu inayowajibika.
Hivi ndivyo alivyoandika
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji,
Africae Munus.
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, Jumapili tarehe 25 Agosti
2013 linaadhimisha Siku ya Makatekista Kitaifa. Uwepo wao ni mchango makini ulioliwezesha
Kanisa Katoliki nchini Brazil kuwafikia watu waliokuwa pembezoni mwa Jamii. Makatekista
wamechangia kwa kiasi kikubwa azma ya Uinjilishaji nchini Brazil. Siku ya Makatekista
Kitaifa nchini Brazil ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na
kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Maadhimisho
haya yanafanyika wakati Kanisa Katoliki Brazil bado lina kumbu kumbu hai ya yale yaliyojiri
katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, Brazil ilipofunikwa
kwa uwepo wa mamillioni ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja ushuhuda
wa imani na matumaini uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.
Maaskofu Katoliki
Brazil wanasema, Katekesi za kina zilizoendeshwa na Maaskofu wakati wa Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani yameacha chapa ya kudumu. Wengi wamejifunza kutoka kwa Baba
Mtakatifu Francisko ambaye kwa wakati huu amekuwa kweli ni kielelezo cha Katekista
mkuu anayefundisha kwa mifano ya ushuhuda wa maisha na maneno yanayoacha chapa ya
kudumu katika maisha ya watu.
Baba Mtakatifu amewagusa wengi kiasi cha kufufua
furaha ya ndani, imani na matumaini ya kusonga mbele bila ya kukata tamaa. Huu ndio
mchango wa Katekesi mang'amuzi ya maisha; Katekesi inayofumbatwa na Neno la Mungu
na Kumwilishwa katika maisha ya Jumuiya ya waamini.