2013-08-22 08:50:06

Papa Francisko ni mtu wa watu kwa ajili ya watu!


Kardinali Jorge Mario Bergoglio, katika uongozi wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, alionesha moyo wa sala na bidii katika maisha na utume wake, akawa ni mfano wa kuigwa katika kusimama kidete kulinda na kutetea maskini na wote waliokuwa wanasukumwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. RealAudioMP3

Ni Baba aliyekuwa na jicho la kuona mahitaji ya jirani zake na moyo thabiti wa kudiriki kuwasaidia kadiri ya uwezo na nafasi yake. Kardinali Bergoglio alionesha karama na maisha ya kitawa katika utekelezaji wa majukumu yake. Ni maneno ya Sr. Nora Antonelli, Mama Mkuu wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina, katika mahojiano maalum na Gazeti la Kila siku la L’Osservatore Romano.

Baba Mtakatifu Francisko katika utume na shughuli zake za kichungaji, alitoa kipaumbele cha pekee kwa majiundo na maisha ya kitawa. Alipenda kukutana na kuzungumza na watawa kwani alitambua kwamba, hawa ni wadau muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Si mtu aliyependa makuu, hata katika matukio makuu ambamo ulitegemea kumwona miongoni mwa viongozi waliokuwa wamepewa viti vya mbele, lakini, wengi walishangazwa kukutana naye kati ya watu wa kawaida.

Kwa maneno mengine anasema, Sr. Nora Antonelli ni kiongozi aliyependa kuwa kati ya watu pasi na makuu! Jambo hili liliwagusa wengi, hali ambayo inaendelea kujionesha hata wakati huu, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hajabadilika hata katika utume wake mpya, bado ni kiongozi anayeonesha unyenyekevu unaosheheni moyo wa upendo na utulivu wa ndani, kwa hakika ni kiongozi anayejiamini katika maisha na utume wake.

Aliwagusa na kupendwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Buenos Aires hasa wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, watu wengi walipokuwa wanashangaa kuona umati mkubwa wa vijana wakiandamana kwa amani na utulivu, huku wakiimba kwa furaha wakati wa Maandamano ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu. Alipenda kuwaonjesha vijana mafundisho tanzu ya imani kwa Katekesi ya kina iliyokuwa inaacha chapa ya kudumu katika miyo ya watu wengi!

Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos, aliwagusa wengi kutokana na mahubiri yake, mafupi lakini ya kina! Barua zake za kichungaji anasema Sr. Nora Antonelli zilikuwa ni mwaliko wa kumfungulia Kristo malango ya maisha kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Huu ulikuwa ni mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini Argentina na wala si kwa ajili ya watu wachache tu ndani ya Kanisa! Alikuwa anakazia huduma ya upendo inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; huduma inayoboreshwa kwa njia ya: Sala na Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Hiki anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji kwa: maskini, wazee, wagonjwa na watoto.

Kardinali Bergoglio alitambua shida na mahangaiko ya Mashirika ya kitawa Jimboni mwake, lakini daima alikuwa tayari kuwafariji na kuwatia moyo kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na mahangaiko yao! Wengi anasema Sr. Nora Antonelli, Mama Mkuu wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Buenos Aires, wameendelea kuimarishwa kwa maneno na mifano yake ya maisha!

Kardinali Bergoglio kama Askofu na mtawa, kila mwaka alikuwa na utamaduni wa kuwaalika watawa kwa ajili ya kujadiliana na kushirikishana mang’amuzi na vipaumbele vya maisha ya kitawa katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji Jimboni mwake. Mkutano wake na watawa ulikuwa unahitimishwa daima na Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini kabla ya Misa, alikuwa anatumia muda mrefu kuzungumza na kufahamiana na watawa, akiomba sala kutoka kwao, unyenyekevu ambao ameendelea kuuonesha tangu siku ile ya kwanza alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kama Askofu mkuu, alipenda kuwaona watawa wanaofanya shughuli za kichungaji Jimboni mwake, wakionesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; daima wakiwa mstari wa mbele kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Tarehe 8 Septemba, kila Mwaka, Kanisa Katoliki nchini Argentina linaadhiisha Siku ya Watawa. Hili lilikuwa ni tukio la pekee kabisa kwa Kanisa Katoliki Argentina kuonesha moyo wa upendo pamoja na kuthamini mchango unaotolewa na Watawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Ushuhuda wa kweli unaojikita kwa Kristo Mwamba thabiti ndiyo furaha ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatamani kuiona ikibubujika kutoka kwa watawa wanapotekeleza utume wao! Wawe na moyo wa: imani, matumaini na mapendo kwa watu wanaowahudumia hasa katika sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu.

Sr. Nora Antonelli anasema kwamba, Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, lilianzishwa na Mama Eufrasia Iaconis. Aliwapenda Watawa wa Mama Eufrasia. Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Machi 2013, wakati macho na masikio ya watu wengi yalikuwa yameelekezwa kwenye Kikanisa cha Sistina mjini Vatican, siku hiyo, Mama Kanisa alikuwa anafanya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Eufrasia, Bikira na Shahidi.

Kardinali Jorge Mario Bergoglio ndiye aliyehitimisha mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Eufrasia Iaconis kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 2 Agosti 2012, kwa mara ya kwanza aliwaambia kwamba, alipata kusikia ushuhuda wa maisha ya Mama Eufrasia kunako mwaka 1953, alipokuwa na umri wa miaka 17 tu! Tangu wakati huo, ule ushuhuda haukuweza kufutika akilini mwake. Alikuwa ni mwanamke wa kawaida lakini aliyebahatika kuwa na karama na vipaji vingi.

Kwa ufupi, huu ndio ushuhuda wa Sr. Nora Antonelli kuhusu maisha na utume wa Kardinali Jorge Mario Bergoglio, Baba Mtakatifu Francisko!

Makala hii imehaririwa na
Padre Richard Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.