Baada ya kuwa tumemtambua Kristo Nuru ya uzima, na kwamba haitoshi kuwepo tu duniani
bali tunapaswa kuandamana naye ili tuwe na uzima, napenda leo tuone tofauti ya ufahamu
wa kibinadamu na ufahamu ndani ya Kristo. Bila shaka unang’aa
jicho ukijiuliza kwa nini mada hii ya leo. Jibu lipo, karibu tuambae pamoja ndani
ya viunga vya Radio Vatican katika makala hii ya vijana. Kwa karne kadhaa sasa
binadamu amekuwa na tabia ya kujiamini zaidi akili yake na uwezo wake wa kuvumbua,
kufahamu na kutenda. Mwanafalsafa Nitsche alikuwa akimshauri dada yake Elisabeth kuwa
jasiri na kujitafutia njia binafsi kwa kutegemea akili zake ili kufahamu mambo, kwani
ndiyo namna nzuri ya kuwa mfuasi bora wa ukweli. Sishangai yawezekana hata wewe
leo ndivyo unavyodhani. Unaona unaweza kufahamu ukweli juu ya ulimwengu, maisha, mafanikio
kwa kutegemea akili na uwezo wako. Kwa hivi unaona imani kwa Mungu ni kama ulemavu
wa fikra au uzembe wa kutafuta mafanikio. Kama na wewe unadhani hivyo basi umebugi
rafiki yangu. Ngoja nikupe mistari ya kweli kuhusu ufahamu na mafanikio. Tumesema
Kristo ni Nuru ya ulimwengu, yeye ni Muumba. Kumbe ina maanisha yeye aliyeumba vitu
vyote ndiye anayefahamu ukweli kuhusu hivyo vitu. Kama formula ya Coca Cola vile,
watu wanahangaika kuitafuta, lakini ni siri ya wachache waliovumbua na waliochanganya.
Hata hivyo Mungu anajua yote hayo. Ukitaka kufahamu ukweli halisi wa vitu na mambo,
mwamini na andamana na Kristu. Kwa akili yako unaweza kufahamu fahamu vijimambo,
au kwa uwezo wako unaweza kujipatia vimafanikio vya hapa na pale ukajiona basi na
wewe babu kubwa, ukajiona pedeshee fulani. Ukweli ni kwamba ufahamu wako ni hafifu,
sio kamili na mafanikio ni ya muda au hata ni halamu. Namaanisha wale mnaotumia njia
zisizo halali kujipatia mafanikio. Hii ni kwa sababu peke yako, kwa nguvu za kibinadamu
huwezi kupata mafanikio au ufahamu unaoridhisha. Hapo unakuwa unaishi gizani, unahitaji
Nuru ya kweli, ambayo ndiyo ninayokuzungumzia hapa, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu Aliye
Hai. Unafanya mchezo nini wewe. Tutazame wale tunaishi katika imani ndani
ya Kristu, tunafahamu mambo kibao, tunaridhika, tuna furaha na tuna amani. Unaelewa
tofauti ipo wapi, ngoja nikutonye kidogo. Baba Mtakatifu Francisko anasema pale
ufahamu na uwezo wa binadamu unapofika kikomo, Nuru ya Kristo inahitajika kuangaza
undani wa mambo na kumtia nguvu mwanadamu (Rej. Lumen Fidei, 3). Na hii ametukumbusha
kule Rio de Janiero, Brasil wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013. Baba Mtakatifu Francisko anasema, bila Nuru ya Kristo huwezi kutambua
na kutofautisha kwa usahihi kati ya wema na uovu. Kwa hiyo ni rahisi kwa kijana kufakamia
mambo ya ajabu, starehe zilizo hatarishi, ulevi, matumizi haramu ya dawa za kulevya
na kadhalika. Tuliza nafsi, mwamini Kristo, utaepuka uovu, utakuwa mwema, utapata
mafanikio, utaridhika na kile ulicho nacho, utakuwa na amani na furaha. Mpaka
hapo umeionaje mistari yangu kuhusu Nuru hii, Kristo Mwenyewe. Unanichezea sauti ya
kinabii wewe, ntakunasa, na utaongoka tu. Basi kwa leo sina la ziada, tuonane tena
makala ijayo. Kutoka Studio za Radio Vatican, ni Padre Celestine Nyanda.