2013-08-22 11:31:56

Haki, amani na upatanisho ni mikakati ya ujenzi wa Nigeria mpya!


Viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Nigeria wanawaalika waamini na wananchi wa Nigeria wenye mapenzi mema, kushikamana kwa pamoja ili kuanza mchakato wa ujenzi wa Makanisa na Misikiti iliyochomwa moto na kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram, kama alama ya upatanisho na mshikamano wa kitaifa.

Ombi hili limetolewa na viongozi wakuu wa kidini nchini NIgeria hivi karibuni, wakati wa majadiliano ya haki, amani na upatanisho yaliyohudhuriwa na viongozi hao! Viongozi wa kidini nchini Nigeria wanasema, wanataka kuwa ni kielelezo cha ujenzi mpya wa Nigeria inayosimikwa katika umoja, upatanisho na mshikamano wa kitaifa.

Viongozi hao wamekazia umuhimu wa elimu makini na majadiliano endelevu kati ya Wakristo na Waislam ili kufahamiana na kushirikiana zaidi na kamwe imani za dini zao zisiwe ni kikwazo cha ujenzi wa amani na umoja wa kitaifa. Kinzani na migogoro ya kikabila na kati ya wakulima na wafugaji ni jambo ambalo limepitwa na wakati. Wakulima na wafugaji wanapaswa kuheshimiana na kusaidiana katika ujenzi na ustawi wa nchi yao.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2007, kuna Wakristo zaidi ya 900 wamepoteza maisha yao kutokana na madhulumu ya kidini na Makanisa 100 yamechomwa moto au kuharibiwa vibaya na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram.







All the contents on this site are copyrighted ©.