2013-08-22 09:18:33

Bikira Maria Malkia wa mbingu, utuombee!


Tarehe 22 Agosti, kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, Siku kuu iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1955. Hii ni kumbu kumbu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, siku chache baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti.

Bikira Maria anashiriki utukufu na ufalme wa Kristo na kwamba, Mama Kanisa anapenda kumweka mbele ya macho ya waamini kama kielelezo makini na mfano wa matumaini ya kwa Wakristo wote ambao pia wanashiriki katika: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kumbu kumbu hii kwa Mwaka wa Imani ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusimama kidete katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika msingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli.

Kanisa bado linaendelea kumwomba Bikira Maria Malkia wa amani aweze kuwaombea walimwengu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, migogoro na kinzani za kijamii, ili watafute amani na kuikumbatia, kwani amani ni jina jipya la maendeleo na ustawi wa wengi.All the contents on this site are copyrighted ©.