Zingatieni ukweli, uaminifu na umakini katika taarifa zenu!
Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox nchini Misri katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari
lina laani vitendo vyote vinavyofanywa kinyume cha maisha ya kiroho, kimaadili na
kiutu na kwamba wananchi wote wanapaswa kusimama kidete kupinga vitendo hivi vinavyohatarisha
maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Misri katika ujumla wao.
Viongozi
wa Kanisa hili wanaendelea kuwaombea wote waliofariki dunia kutokana na machafuko
ili wapate pumziko la milele; majeruhi waweze kupona haraka na kurudi tena katika
shughuli zao za kila siku, huku wakipania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani
na utulivu. Viongozi hawa wanavitaka pia vyombo vya habari vya kimataifa kuhakikisha
kwamba, vinatekeleza wajibu wao barabara kwa kuzingatia misingi ya: ukweli, uaminifu
na umakini.
Wanawaomba wananchi wa Misri kujikita katika mchakato wa majadiliano
ya kina na upatanisho wa kweli ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kanisa la Kikoptik linalaani mauaji ya askari kuwa ni kitendo cha kinyama kwani hawa
walikuwa wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa taifa. Viongozi hao wanasema, wasingependa
kuona mataifa ya nje ya kiingilia mambo ya ndani ya Misri kwa hali inaweza kuwa ni
mbaya zaidi.
Kama viongozi wa Kanisa wanatumaini huruma na ulinzi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, atakayewaimarisha na kuwawezesha kujenga tena nchi yao upya katika
misingi ya haki, amani, utulivu na demokrasia ya kweli.