2013-08-21 08:07:15

Uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja katika teknolojia ni chachu ya maendeleo endelevu kwa nchi maskini duniani


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni katika mkutano wa Shirika la Biashara Duniani aliwapongeza wadau mbali mbali wa shirika hili kwa kutekeleza majukumu yao huku wakizingatia utu na maadili. RealAudioMP3
Nchi Changa zaidi duniani ni kiungo dhaifu sana katika Jumuiya ya Kimataifa, lakini zina idadi ya watu wapatao millioni 880, kiasi cha asilimia 12% ya idadi ya watu duniani, lakini wanachangia kiasi cha asilimia 2% ya Pato Ghafi la Dunia, kiasi cha asilimia 1% cha biashara duniani.
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anabainisha kwamba, mchango huu hafifu kutoka katika Nchi maskini zaidi duniani unatokana na ukweli kwamba, uchumi na maendeleo yao bado yakon yuma kutokana na ujuzi hafifu, ugawaji mbaya wa rasilimali na pato la taifa pamoja na ukosefu wa mapato ya ndani ambayo yangeweza kuchangia katika mchakato wa maboresho ya hali ya uchumi na biashara katika nchi hizi.
Mikakati mbali mbali ya maendeleo iliyobuiniwa kwa miaka ya nyuma, inaonekana kutofua dafu na kwamba, watu wengi wameendelea kutumbukia katika balaa la umaskini wa hali na kipato na kwamba, ubora wa maisha ya wananchi wengi unaendelea kufifia mwaka hadi mwaka kadiri ya takwimu kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Tangu mwaka 2002 hadi mwaka 2007 kumekuwepo na ongezeko la maskini wapatao millioni tatu kila mwaka.
Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2007, asilimia 59% ya watu Barani Afrika walikuwa wanaishi kwa kiwango cha dolla 1.25 kwa siku. Pato la kila mwananchi linaendelea kupungua siku hadi siku na kwamba, asilimia 50% ya wananchi wanaoishi katika nchi changa zaidi duniani wanakabiliwa na umaskini mkubwa na kwamba, hakuna matumaini ya maboresho ya hali ya wananchi hawa ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitachukua hatua za dharura.
Nchi nyingi zinaweza kushindwa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa sababu ya uzalishaji na tija kuwa ni katika kiwango cha chini kabisa; miundo mbinu hafifu na kwamba, kuna kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi unaoendelea kufyeka nguvu kazi ambayo ingeweza kutumika kuzalishia mali na kutoa huduma. Takwimu za ugonjwa wa Ukimwi zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2011 kulikuwa na wagonjwa wa Ukwimwi duniani wapatao millioni 34, kati yao millioni 9.7 wanatoka katika nchi changa zaidi duniani.
Wagonjwa millioni 4.6 walikuwa wanahitaji kupatiwa dawa za kurefusha maisha, lakini ni wagonjwa millioni 2.5 tu ndio waliokuwa wamefanikiwa kupata dawa hizi. Hii ina maana kwamba, wagonjwa wengi wa Ukimwi hawana tena matumaini ya kuendelea kuishi. Bado kuna magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanawanyemelea wananchi katika nchi maskini zaidi duniani kwa kasi kubwa kuliko ilivyo katika nchi tajiri zaidi duniani.
Askofu mkuu Silvano Tomasi anasema kwamba, Nchi maskini duniani zinataka ziwezeshwe ili ziweze kujikwamua kutoka katika mkwamo wa uchumi na maendeleo, ili hatimaye, waweze kuung’oa umaskini ambao umekuwa ni kizingiti kikubwa cha maendeleo ya wananchi. Anasema, miliki ubunifu inapaswa kupimwa kwa kuangalia faida na maendeleo yanayoweza kupatikana kwa Nchi changa zaidi duniani, ikiwa kama zitasaidiwa kupata teknolojia; kwa kuzingatia haki na wajibu.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu umesisitizia kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, miliki ubinifu inatumika kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kujenga uhusiano mwema katika Jumuiya ya Kimataifa na kwa namna ya pekee na Nchi changa zaidi duniani. Miliki ubunifu iwe ni kikolezo cha mchakato wa maboresho ya maendeleo na uchumi. Uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano wa kiteknolojia ni chachu ya maendeleo endelevu kwa nchi maskini zaidi duniani.
All the contents on this site are copyrighted ©.