Tarehe rasmi ya kuwatangaza Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu kujulikana
rasmi hapo tarehe 30 Septemba 2013
Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 30 Septemba 2013 anatarajiwa kutangaza tarehe
rasmi kwa siku ambayo amechaguwa ili kuwatangaza Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane
Paulo II kuwa kwenye orodha ya watakatifu wa Kanisa. Hayo yamebainishwa na Kardinali
Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri
na watakatifu wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican.
Baba Mtakatifu siku
hiyo, atakuwa na mkutano wa kawaida na Makardinali kutoka sehemu mbali mbali za dunia
ili kujadili ombi la kuwatangaza waamini walionesha mifano bora ya kuigwa katika maisha
na utume wao ndani ya Kanisa. Ni Baba Mtakatifu peke yake ambaye kwa sasa anafahamu
tarehe hiyo maalum, kinyume cha baadhi ya taarifa zilizokuwa zimeenea kwenye vyombo
mbali mbali vya habari kwamba, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili angeweza kutangazwa
mwaka huu.
Kardinali Angelo Amato anasema, Mwenyeheri Yohane wa XXIII alikuwa
Nabii na Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Mwenyeheri Yohane
Paulo II akafafanua na kumwilisha Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican katika
maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Viongozi hawa wawili ni miamba
wa utamaduni na utakatifu wa maisha ya Kikristo.