2013-08-21 10:23:02

Mwaka wa Imani na Ibada maalum kwa Bikira Maria: 12-13 Oktoba 2013


Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI, Kanisa katika Mwezi Oktoba litaadhimisha Mwaka wa Imani kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Kuanzia tarehe 12 hadi 13 Oktoba, kutakuwa na Maadhimisho maalum ambayo yatamshirikisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vyama vyote vya kitume vinavyochota tasaufi yake kutoka kwa Bikira Maria. Tukio hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji mpya. Hii ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 10 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Tukio hili ni sehemu ya kumbu kumbu ya Bikira Maria alipowatokea watoto watatu wa Fatima yaani: Francisko, Yacinta na Lucia, hapo tarehe 13 Oktoba 1917. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima italetwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili waamini na watu wenye mapenzi mema waweze kutoa heshima yao kwa Bikira Maria wa Fatima.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, hapo tarehe 12 Oktoba 2013 kuanzia Saa 2:00 asubuhi kwa saa za Ulaya, waamini watafanya hija kuzunguka kaburi la Mtakatifu Petro, watapata nafasi ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho kutoka kwenye Makanisa yanayolizunguka Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Jioni saa 11:00. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kupokea Maandamano ya Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na hapo Baba Mtakatifu atatoa Katekesi ya kina kuhusu Ibada kwa Bikira Maria. Sanamu hii itapelekwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria ya "Divino Amore" hapa Roma kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu, itakayowaunganisha waamini kutoka kwenye Madhabahu ya Bikira Maria yaliyotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Saa 4:00 Usiku, kutafanyika kesha la Sala kwa Bikira Maria.

Jumapili tarehe 13 Oktoba 2013, Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima itarudishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Saa 4: 30 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu. Askofu mkuu Rino Fisichella anasema, Ibada hii ni utashi ulioneshwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya heshima na ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ana ibada ya pekee kwa Bikira Maria, ambaye hivi karibuni alijiweka chini ya ulinzi na usimamizi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.