2013-08-21 15:31:33

Jengeni utamaduni wa majadiliano ili kudumisha haki na amani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 21 Agosti 2013 amekutana na Kundi la wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Seibu Gauken Bunri kutoka Tokyo, Japan waliofika kutembelea Makumbusho ya Vatican.

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kumtembelea pamoja na kutembelea Vatican katika ujumla wake, kwani ziara kama hizi ni fursa makini zinazowawezesha wanafunzi kukutana na kufahamiana na watu mbali mbali, ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa kitamaduni. Dhana ya kukutana na watu wenye misimamo, tabia, tamaduni na imani tofauti inawajengea uwezo wa utamaduni wa majadiliano kama sehemu ya ukomavu wa mtu mzima kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano yana athari zake kwani yanaweza kusababisha kinzani na migogoro, lakini majadiliano ya kweli yanasimikwa katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upendo. Ni changamoto ya kusikiliza kwa makini kabla ya kuzungumza, kwani amani inasimikwa katika msingi wa majadiliano na kuthaminiana. Vita, kinzani na migogoro mbali mbali inayoendelea kuibuka kila siku ni dalili za kukosekana kwa majadiliano ili kujenga amani ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia kheri na baraka katika matembezi yao mjini Vatican na Italia katika ujumla wake. Watoto hao kwa upande wao, wameshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwapokea na kuwasalimia.







All the contents on this site are copyrighted ©.