Umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa njia ya elimu
Kituo cha Kimataifa cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni (Kaiciid) kilichoanzishwa
kwa ushirikiano wa Falme za Kiarabu, Hispania, Australia na Vatican ikiwa ni nchi
mwanachama mtazamaji na mwanzilishi, bado kinaendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni
katika nchi mbali mbali.
Hapo tarehe
26 Agosti 2013, kauli mbiu itakayoongoza Warsha ya siku moja ni “taswira ya mwingine”.
Warsha ambayo itafanyika Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya Bara la Afrika.
Mada
hii inalenga kukuza na kuendeleza elimu na majiundo ya majadiliano ya kidini na kiakili
miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali Barani Afrika. Wajumbe 130 kutoka katika
sekta ya dini na elimu wanatarajiwa kushiriki. Mada hii inatarajiwa kufanyiwa kazi
kwa kipindi cha miaka mitatu. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2013 ni elimu, Mwaka 2014
utajadili kuhusu njia za mawasiliano ya kijamii na mwaka 2015 wajumbe watapembua kwa
kina na mapana ulimwengu wa mtandao.
Mada hii itaendelea kujadiliwa Barani
Asia na Amerika na kuhitimishwa kwa mkutano wa kimataifa utakaofanyika hapo tarehe
18 hadi 19 Novemba 2013 huko Vienna, Austria.
Itakumbukwa kwamba, Kituo cha
Kimataifa cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni kilianzishwa rasmi kunako tarehe
26 Novemba 2012 kwa lengo la kuhamasisha, kurahisisha, kukuza na kujenga majadiliano
ya kidini miongoni mwa wafuasi wa dini mbali mbali duniani, ili kujenga dunia inayosimikwa
katika utamaduni wa ushirikiano, heshima katika tofauti za kiimani, haki na amani.
Mfalme Abdullah Bin Abdulaziz, Mfalme wa Falme za Kiarabu, alipokutana na
kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, hapo tarehe 6 Novemba
2007, aliomshirikisha nia ya kuanzisha Kituo cha Kimataifa kwa ajili ya majadiliano
ya kidini na kitamaduni. Wakati wa uzinduzi wa kituo hiki, Kardinali Jean Louis Tauran,
Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini alimwakilisha Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita katika shughuli hii.
Alisema katika hotuba yake
kwamba, Kituo hiki cha Kimataifa, ilikuwa ni fursa nyeti ya ujenzi wa jukwaa la majadiliano
katika medani mbali mbali za maisha ya waamini. Uhuru wa kuabudu ni mada muhimu sana
kwa waamini wote. Kituo hiki kinatambulika na Umoja wa Mataifa kama Jukwaa na nafasi
ya majadiliano kwa kutoa fursa muhimu kwa watu wenye uzoefu na mang’amuzi makubwa
kuweza kushirikisha matunda ya majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini
mbali mbali.
Akizungumzia kuhusu Kituo hiki cha Kimataifa, Padre Federico
Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican alibainisha kwamba, Vatican inaweza kuchangia kwa
kiasi kikubwa uzoefu na mang’amuzi yake katika majadiliano ya kidini.