2013-08-20 08:00:49

Uchomaji wa Makanisa ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kamwe!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anaendelea kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa nchini Misri ambayo kwa sasa inakabiliwa na hali tete ya machafuko ya kisiasa na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Kardinali Sandri anasema, wananchi wa Misri wanaweza kumaliza hali ya machafuko ya kisiasa nchini humo kwa njia ya majadiliano ya kina pamoja na upatanisho wa kitaifa. Anakumbusha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha bia mwanadamu. Waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Misri. Anapenda kuwatumia viongozi wa Makanisa, waamini na wapenda amani nchini humo salam za mshikamano wa upendo wakati huu wanapokabiliana na hali tete katika historia ya nchi yao.

Kardinali Sandri anasema, vitendo vya kuchoma na kuharibu Makanisa ni jambo ambalo haliwezi kukubalika. Maendeleo na ustawi wa wananchi wa Misri yatategemea kwa kiasi kikubwa mikakati na sera makini katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila binadamu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kiimani na kidini na kwamba, uhuru wa kidini ni nguzo msingi wa haki zote za binadamu.

Kanisa linaendelea kusema kwamba, dini ya kweli haiwezi kuwa ni chanzo cha vita na vurugu au vitendo vya kigaidi; kamwe jeshi haliwezi kutumika kutoa suluhu ya masuala ya maisha ya kidini miongoni mwa waamini wa dini tofauti. Jambo la msingi ni kila mwamini kuhakikisha kwamba, anamwilisha ndani mwake ile amri ya upendo kwa Mungu na jirani bila kuangalia tofauti za kiimani au kiitikadi.







All the contents on this site are copyrighted ©.