2013-08-20 10:12:48

Papa Francisko, bado anaendelea kuwashukuru wenyeji wa Rio de Janeiro!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua ya shukrani Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro kutokana na moyo wa ukarimu waliomwonjesha wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani. Vijana wameonesha nguvu ya imani dhidi baridi na mvua zilizoambatana na Maadhimisho haya.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro, Kamari kuu ya maandalizi na vijana wote waliojitolea kuwahudumia ndugu zao kwa moyo wa upendo na mshikamano, bila kuwasahau wananchi wa Brazil kwa ujumla wao!

Baba Mtakatifu anamwomba Askofu mkuu Tempesta kumfikishia salam zake za upendo kwa vijana wanaopata matibabu kutoka katika Hospitali ya Mtakatifu Francisko wa Asisi ambao alipata bahati ya kuwatembelea na kuzungumza nao, bila kuwasahau wakazi wa kitongoji cha Varginha na Copacabana.

Baba Mtakatifu mwishoni, anamwomba Askofu mkuu amfikishie salam zake za pekee kwa wananchi wa Guaratiba, mji ambao haukubahatika kutumika kwa ajili ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 kutokana na mvua kubwa, iliyosababisha matope kujaa kwenye Uwanja wa Campus Fidei uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya shughuli hizi.All the contents on this site are copyrighted ©.