2013-08-20 07:26:30

Jengeni utamaduni wa majadiliano ya kina ili kudumisha haki, amani na mafao ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Benin katika ujumbe wake kwa Waamini na wananchi wa Benin wakati huu wanapoanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Benin, wanawaalika wadau wote kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa majadiliano ya kina, ili kudumisha misingi ya haki na amani; kwa kuthaminiana na kuheshimiana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa unaopania mafao ya wengi.

Hivi karibuni Rais Yayi Boni wa Benin ameanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini Benin, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa nchini humo kutokana na ukweli kwamba, mabadiliko haya yanapania kumwongezea Rais madaraka pamoja na kuimarisha dhamana ya Mahakama ya Kikatiba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Benin linasema, Kanisa halina majibu ya kiufundi wala kisiasa katika mjadala huu, lakini lina dhamana na utume wa Kinabii na Kimaadili unaolisukuma kuwakumbusha Waamini na wananchi wote wa Benin kwamba, hakuna demokrasia ya kweli inayolenga kuwaganywa watu; bali daima demokrasia uwe ni utawala shirikishi kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Benin.

Wananchi wa Benin kwa sasa wanakabiliana na baa la umaskini wa hali na kipato, lakini kuna baadhi ya wananchi wanaokula na kusaza kutokana na ubinafsi, rushwa na ufisadi, mambo ambayo yanaendelea kuchangia kinzani na migogoro ya kijamii nchini humo. Kuna kundi kubwa la vijana ambalo halina fursa za ajira, hali ambayo inatishia amani na usalama wa wananchi wa Benin. Madai ya kutaka kuipindua Serikali halali iliyoko madarakani ni mambo yanayoendelea kuzua hofu na wasi wasi miongoni mwa raia wenye mapenzi mema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Benin linasema, shida na changamoto zote hizi zinaonesha kwamba, kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kina, kwa kujikita katika huduma bora na makini kwa wananchi wa Benin; kwa pamoja wakitafuta na kudumisha mafao ya wengi, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu wanakumbusha kwamba, si rahisi wala haki kwa baadhi ya wanasiasa kujitwalia madaraka na jukumu la kutaka kutatua matatizo yote ya wananchi wa Benin.

Kuna haja ya kujenga dhamana ya uwajibikaji na mshikamano wa pamoja, kutoka kwa mwananchi, wakuu na wadau wa sekta mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi. Jamii ijikite zaidi katika ukweli, uwazi na uaminifu kwa kuzingatia makubaliano yaliyokwishakufikiwa katika hatua mbali mbali za majadiliano kuhusu mafao na maendeleo ya wananchi wa Benin.

Baraza la Maaskofu Katoliki Benin, linawakumbusha wanasiasa sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Mwezi Novemba 2011, alipokuwa nchini Benin kwa ajili ya kuzindua Matunda ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Afrika, kwa kuwataka wanasiasa na wachumi kutoka Barani Afrika na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, hawathubutu kupokonya matumaini kutoka kwa wananchi wao na wala wasiwe ni kikwazo cha maendeleo yao kwa siku za usoni.
All the contents on this site are copyrighted ©.