2013-08-20 07:15:43

Hali kuhusu mabadiliko ya tabianchi, njaa na utapiamlo!


Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kuhusu: uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa hewa ya ukaa, baa la njaa na utapiamlo, zinaonesha jinsi ambavyo sekta ya kilimo inavyochangia katika masuala haya. RealAudioMP3

Hewa ya ukaa inayozalishwa kutoka katika sekta ya kilimo imeongezeka kwa asilimia 1.6 kwa mwaka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2010.

Hali hii imesababisha ongezeko la hewa ya ukaa angani kwa asilimia kumi; jambo linalochangiwa na kazi zabinadamu. Shughuli za ufugaji na matumizi ya mbolea za viwandani ni kati ya mambo makubwa yanayoendelea kuchangia uchafuzi wa mazingira. Hapa hewa chafu inayozalishwa angani kutokana na janga la uchomaji misitu na matumizi ya ardhi haikuingizwa.

Takwimu za FAO kuhusu: mtaji na uwekezaji; mabadiliko ya tabianchi; upatikanaji wa chakula; uzalishaji wa chakula na biashara; baa la njaa na utapiamlo; athari zake katika hali ya nchi na uhusiano wake na maisha ya binadamu zimechambuliwa kwa kina na mapana. FAO inasema kwamba, ukosefu wa chakula umekuwa pia ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kijamii. Kutokana na changamoto hizi kuna haja ya kuwa ni matumizi mazuri ya rasilimali katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha kwamba, kilimo kinakuwa ni endelevu na rafiki kwa mazingira.

Katika kipindi cha Mwaka 2010 hadi mwaka 2012 kulikuwa na watu millioni 870 waliokuwa wanapata lishe duni. Hii ni sawa na asilimia 12.5 ya idadi ya watu duniani, wengi wao ni wale wanaoishi katika Nchi changa. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2011, nchi nyingi za Kiafrika zilisema kwamba, kuna watu waliokuwa wanakabiliwa na lishe duni hali iliyopelekea watu kudumaa na wengine wengi kuwa na uzito mdogo kuliko kiwango cha wastani. Barani Afrika idadi hii ni sawa na asilimia 20% na kwamba, hali ni mbaya kwa wananchi wanaoishi katika nchi za Pwani ya Pembe.

Takwimu za uzalishaji katika sekta ya kilimo zinaonesha kwamba, uzalishaji umeongezeka maradufu na kwamba, uzalishaji wa mazao ya nafaka umeongezeka zaidi kwani hiki ni chakula kinachotumiwa zaidi na watu wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani. Uzalishaji huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini China na India. Nafaka ni chakula ambacho kwa sasa kinatumika pia kama nishati uoto! Hali ya uchumi inabainisha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la ununuzi wa chakula unaofanywa na Serikali, hasa kutoka katika nchi zinazoendelea. Ongezeko la bei ya mazao ya nafaka imeongezeka kwa asilimia 4% na hivyo sekta ya kilimo imechangia asilimia 1% ya Pato Ghafi la Dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.