Mungu
anamtokea Gideoni, Mwamuzi (Judge) wa kwanza baada ya kifo cha Joshua ili afanye kazi
yake ya kuwaongoza kwa muda Waisraeli. katika vita. Visingizio vya unyonge wa Gideoni
kuwa ni kutoka kabila dhaifu na wa mwisho katika familia yake, vilitolewa hata na
Musa (sijui kuongea), Yeremia (mimi ni mdogo) na Isaya (nina midomo michafu). Kazi
ya Mungu haitegemei akili zetu, nguvu zetu, ufundi wetu - bali unyoofu na ukubali
wetu. Roho wa Mungu atatujalia cha kusema na cha kutenda kama zawadi iliyoshuka siku
ya Pentekoste kwa mitume.
Mungu anamchukua kamanda wa mgambo, askari asiye
mzoefu, mtu mshamba wa kijijini. Mungu anajua mapungufu yote ya Gideoni lakini bado
anamchagua na kuwekeza wito wote huu katika chombo cha udongo. Mungu anamjenga kisaikolojia
Gideoni kuwa atakuwa naye daima katika vita na uongozi wake. Sadaka anayotoa Gideoni,
Mungu anaishiriki kwa kutuma moto uiteketeze.
Somo la Injili : (Mt 19:23 -
24)
Ni rahisi kwa ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika
ufalme wa mbinguni. Mitume wanashangaa sana. kristu anawashusha wasi wasi wao na kuwaambia
kuwa hii kwa Mungu inawezekana (Mt 19:26).
Masomo yetu ya leo Agosti 20, 2013
yanatuambia :
1. Mungu wetu akitupa kazi yake huwa hatuachi peke yetu - "nipo
pamoja nanyi hadi ukamilifu wa dahari.."(Mt 28:20). Mungu hatuachi peke yetu katika
mapambano ya ndoa zetu. Mungu daima anawasindikiza wana ndoa na kuwafanyia miujiza
pale tunapomwalika Kristu kama walivyofanya wale wa harusi ya Kana (Yoh 2:1 - 11).
Shida tuipatayo katika ndoa zetu ni pale ambapo tunapowaalika wazazi na mashangazi
zetu tu wakati tunapotofautiana. Kristu akiwa kati yetu tutaweza kusikia sauti yake
ndogo - msamehe mwenzako.. !
2. Kujipunguza, kujiachia na kujibandua katika
mali zetu ni kupata mara mia hapa duniani na uzima wa milele mbinguni. Hii haimaanishi
kwamba kuwa tajiri ni kitu kibaya au ni dhambi, ila kwamba Kristu anataka tujijenge
katika moyo wa ukarimu. Mtume Paulo aliwasifu sana Kanisa la Wafilipi kwa utajiri
wao wenye kusheheni ukarimu, kwa kusaidia Kanisa la Yerusalem (Wafilipi 4:14-20).
Wema daima huwa hauozi. Tujisikie faraja na fahari tunapowasaidia wengine wenye shida.
Tusali
kwa kuomba roho ya ukarimu kwa familia zetu. Pia tuombee kazi zetu ambazo wakati mwingine
zinazidi kimo na uwezo wetu.
Tafakari hii inaletwa kwako kwa njia ya mtandao
na Padre Beno Michale Kikudo, Jimbo kuu la Dar es Salaam.