2013-08-19 09:24:12

Tafuteni mambo ya msingi zaidi, gundueni njia na mbinu za Uinjilishaji mpya!


Mkutano wa 34 wa urafiki kati ya watu wa Mataifa kwa mwaka huu unaongozwa na kauli mbiu "dharura kwa binadamu" na changamoto kubwa katika azma ya Uinjilishaji kwani Kanisa linatambua kwamba, binadamu ndiye njia inayotumiwa na Mama Kanisa hata katika ulimwengu wa utandawazi, kila mwamini anaalikwa kugundua utume wake na kujikita zaidi katika mambo msingi, daima akitafuta njia na mbinu mpya za Uinjilishaji.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa urafiki kati ya watu wa mataifa uliofunguliwa rasmi hapo tarehe 18 Agosti na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 24 Agosti 2013, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tracisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Ujumbe huu umesomwa na Askofu mkuu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki Rimini, Italia wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano huu, Jumapili iliyopita.

Binadamu anaendelea kuwa ni fumbo la uhuru, neema, ufukara na ukuu. Ni njia inayotumiwa na Mama Kanisa katika utekelezaji wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale; kwa namna ya pekee utu na heshima ya binadamu vinajionesha kwenye Fumbo la Umwilisho, linalomwonesha Kristo kuwa ni ukweli na njia ya maisha. Ni mlango uliofunguliwa kwa ajili ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanadamu bado ni mdau mkubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kwa ajili ya njia za mawasiliano ya kisasa, ndiyo maana mwanadamu amekuwa ni sawa na "kichwa cha mwendawazimu" kila mtu anataka kukifanyia majaribio ili kuharibu uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu unaowafanya binadamu kuwa huru jambo ambalo ni kikwazo kwa wale wasiowatakia mema binadamu.

Mkutano wa Rimini unapania kutoa tafakari ya kina inayomrudishia mwanadamu utu na heshima yake, tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuheshimu na kuthamini utakatifu wa maisha ya mwanadamu, ili kila mtu aweze kutekeleza kwa ukamilifu utume wa maisha yake. Kristo amelidhaminisha Kanisa: Injili, Sakramenti na kwamba, Kanisa ni chemchemi msingi ya matumaini ya mwanadamu, changamoto kwa waamini kuwaendea wote wenye kiu ya kutaka kukutana na kumfahamu Mwenyezi Mungu.

Waamini wajitahidi kumuiga Yesu aliyejifanya mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ili kuwa karibu na kila mtu na katika medani mbali mbali za maisha, ili wote waweze kuonja upendo wa Mungu. Waamini wanachangamotishwa kuwa na ujasiri wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu bila woga wala makunyanzi; wakati ufaao na wakati usiofaa kwa kuzingatia ukweli na heshima.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni wajibu wa kila mwamini anayetumwa kumhudumia mwanadamu, akijitahidi kumwendea pembezoni mwa maisha yake ya kijamii na kiroho alikojificha. Waamini wanapaswa kuwa ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuweza kutekeleza utume wa Mama Kanisa kama Mama na Mwalimu; wakionesha utii katika ukweli, ili watu waweze kumrudia Kristo na kujifunza kutoka kwake, kwani Yeye ndiye njia, ukweli na uzima.

Ni mwaliko wa kuwaendea wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii hasa maskini wa hali na maisha ya kiroho. Hawa ni maskini wanaotindikiwa upendo; wenye kiu ya ukweli na haki; watu wanaomtafuta Mwenyezi Mungu, ili waweze kumpeleka kwa jirani zao.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, tafakari hii inaweza kuwa ni msaada mkubwa wakati huu wajumbe wa mkutano wa 34 wa urafiki kati ya watu wanapokutanika mjini Rimini ili kufanya tafakari ya kina kuhusu dharura ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka yake takatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.