Kanisa linahamasisha utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi
Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani ilikuwa ni fursa nyingine kwa vijana kuweza
kujinoa kuhusu mada mbali mbali katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya
haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira, dhamana ambayo Mwenyezi Mungu
amemkabidhi mwanadamu. Kanisa linapenda kukazia kuhusu dhana ya utunzaji wa mazingira
kadiri ya Mafundisho ya Kanisa.
Itakumbukwa
kwamba, kunako mwaka 1992 Jumuiya ya Kimataifa ilianzisha mchakato unaopania kudumisha
maendeleo endelevu, uliofanyika huko Rio. Maendeleo endelevu ni dhana inayobainisha
maendeleo yanayogusa mahitaji ya watu wa kizazi hiki bila kuhatarisha maisha ya kizazi
kijacho.
Kunako mwaka 2012, Jumuiya ya Kimataifa ikakuyakutanisha Mataifa
makubwa yaliyokuwa yanaibukia katika kasi kubwa ya maendeleo ili kutafuta mbinu mkakati
wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo endelevu, mkutano huo ukaitwa Rio+20. Kwa bahati
mbaya, mkutano huu ukahitimishwa pasi na ufafanuzi makini wa utekelezaji wa malengo
ya maendeleo endelevu katika Jumuiya ya Kimataifa.
Ni mchango wa Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anachangia
kwenye kongamano la utunzaji bora wa mazingira wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28
ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Anasema, Mababa watakatifu wamekuwa wakikazia
kwa namna ya pekee utunzaji bora wa mazingira kama msingi wa kuendeleza haki na amani
duniani, kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.
Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Upendo katika
Ukweli, “Caritas in Veritatis”, anaeleza kwamba, maendeleo endelevu ni changamoto
inayomtaka kila mtu kuwajibika kadiri ya nafasi na dhamana yake, ili dunia iweze kuwa
ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Papa Francisko alipokuwa anazungumza na Waandishi
wa habari siku chache tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alibainisha
kwamba, ameamua kuchagua jina la Francisko kwani ni Mtakatifu aliyesimama kidete kulinda
na kutunza mazingira.
Hii ni changamoto kwa kila mtu kulinda mazingira kwa
ajili ya mafao ya wengi. Lakini, mwelekeo wa sasa ni watu kutaka kujinufaisha wenyewe,
kiasi cha kuhatarisha amani, maendeleo na ustawi wa wengi. Mafundisho ya Kanisa kuhusu
utunzaji bora wa mazingira yanapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, kama
hali inayoonesha uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu kama sehemu ya mchakato wa kudumisha
haki, amani na ustawi wa wengi.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita katika ujumbe wake kwa Siku ya kuombea amani duniani kwa mwaka 2010 alisema ukitaka
kuvuna amani, linda mazingira, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kutunza mazingira kama kielelezo makini cha amani.
Kardinali Turkson anasema
kwamba, Biblia ni kitabu ambacho kinatoa dira na mwongozo wa utunzaji bora wa mazingira
kwa mtu binafsi, familia na Jamii husika, kwa kuzingatia maadili, tasaufi, haki na
wajibu wa kijamii. Lengo ni kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana
na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kutishia amani na usalama kwa Jumuiya
ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linawajibu na dhamana ya kuendelea
kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira kama kikolezo cha amani duniani.
Vijana
wanapaswa kurithishwa utamaduni wa kupenda, kulinda na kutunza mazingira kwa ajili
ya mafao yao kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Vijana wanakumbushwa kwamba,
wamepewa dhamana ya kutunza mazingira na maisha yao kwa ujumla. Ni mwaliko wa kuachana
na utamaduni unaokumbatia kifo, mambo yanayoharibu ekolojia ya maisha ya mwanadamu
kutoka katika undani wake. Jamii inahamasishwa kutunza mazingira kwa ajili ya mafao
ya wengi. Mazingira pia ni kielelezo cha zawadi ya Mungu kwa binadamu, kama yalivyo
maisha.
Ni matumaini ya Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa
la Haki na Amani kwamba, vijana wataendelea kuwahamasisha vijana wenzao kusimama kidete
kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi.
Imehaririwa na Padre
Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.