2013-08-19 10:44:24

Jaji Warioba: Hutushawishi Wananchi, Tunafafanua


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesema Tume yake haishawishi wananchi wakubali mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba waliyoiandaa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu lakini hulazimika kutoa ufafanuzi pale inapohitajika.

Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo mjini Morogoro Jumamosi, Agosti 17, 2013, wakati akijibu swali la mmoja wa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Manispaa ya Morogoro aliyeomba ufafanuzi wa Tume kuhusu kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Tume yake inashawishi Wajumbe wa Mabaraza kukubali rasimu ya Katiba.

“Mna haki ya kuuliza na kupata ufafanuzi na sisi kama Tume tuna wajibu wa kutoa ufafanuzi kwa yale mnayouliza katika mikutano … huo sio ushawishi ni ufafanuzi,” alisema Mwenyekiti huyo akijibu swali la mjumbe huyo Bw. Dotto Rangimoto.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Wajumbe wa Tume wanaoendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba nchini huulizwa maswali mbalimbali na wananchi wanaohudhuria mikutano hiyo wakitaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyomo katika rasimu ya katiba.

“Tusipojibu tutakuwa watu wa ajabu sana,” alifafanua Mwenyekiti huyo katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mjini Morogoro.

Ufafanuzi wa Itikadi ya Ujamaa ndani ya Katiba

Katika mkutano huo, Jaji Warioba pia alifafanua kuhusu misingi ya ujamaa na kujitegemea katika rasimu ya katiba iliyoandaliwa na Tume yake. Jaji Warioba amesema Tume yake imependekeza katika rasimu ya katiba uwepo wa Dira na Malengo ya Taifa ambayo yatapaswa kutekelezwa na serikali ya chama chochote kitakachokuwa madarakani.

“Ujamaa ni itikadi lakini kujitegemea sio itikadi … na baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, tulikubaliana kuwa vyama vitakuwa na itikadi tofauti,” alisema Mwenyekiti huyo na kufafanua kuwa mapendekezo ya Tume yake yanalenga kutekeleza malengo ya taifa na sio itikadi ya chama chochote kitakachokuwa madarakani.

Ufafanuzi wa Jaji Warioba ulitokana na swali la Mjumbe wa Baraza hilo Bw. Andrew Tarimo aliyetaka kujua itikadi ya inayopendekezwa na Tume baada ya ile ya ujamaa na kujitegemea kuondolewa katika rasimu iliyoandaliwa na Tume na kuzinduliwa Juni 3 mwaka huu.

“Rasimu imeweka dira na malengo ambayo yatasimamiwa na chama chochote bila kujali itikadi ya chama hicho,” alisema. Baraza la katiba la Manispaa ya Morogoro limemaliza mkutano wake wa siku tatu yaani Jumamosi, Agosti 17, 2013) uliohudhuriwa na wananchi 155 kutoka kata 29 za Manispaa hiyo. Jumatatu, Agosti 19, 2013 Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro nalo linatarajiwa kuanza mkutano wake wa siku tatu kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba.








All the contents on this site are copyrighted ©.