2013-08-19 08:47:15

Imani inawajibisha na wala si kama urembo uliopambwa kwenye keki!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Agosti 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewataka waamini kuwa na subira katika majaribu na kuendelea kumtumainia Yesu Kristo, chanzo na kilele cha imani yao.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaalikwa kumtaza Yesu Kristo ili kujenga na kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu. Yesu ni daraja muhimu sana kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu, kwani Yesu ni Mwana Mpendwa wa Mungu na waamini ni ndugu zake Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu kwa Jumapili ya Ishirini ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inachangamoto kubwa ambayo inapaswa kuangaliwa kwa makini kutokana na ugumu wake. Yesu anawauliza wafuasi wake, Je, mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Moto unaozungumzwa na Yesu anasema Baba Mtakatifu ni imani ambayo imeletwa na Yesu hapa duniani, inayomtaka mwamini kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha yake, kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo.

Kwa njia ya Yesu, waamini wanapata fursa ya kuweza kumtambua Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na upendo; mkweli na mwaminifu na kwamba, ni chemchemi ya maisha kwa ajili ya wote. Kutokana na mantiki hii, Yesu anasema amekuja kuleta mgawanyiko kati ya watu, kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe ndiye kiini cha amani na upatanisho wa kweli.

Amani inayoletwa na Yesu inamtaka mwamini kumkana Shetani na mambo yake yote; kuachana na ubinafsi, ili hatimaye, kuchagua jema, ukweli na haki hata pale ambapo mambo haya yanahitaji sadaka kubwa pamoja na kujitosa kimasomaso. Mambo haya yanaweza kuwagawa watu, lakini, Yesu ni daraja linalowaunganisha watu na wala si kinyume chake.

Yesu anawapatia wafuasi wake vigezo msingi vya kufanya maamuzi yao katika maisha: kuishi katika ubinafsi au kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza; kutumikiwa au kutumikia wengine; kutii ubinafsi au kumtii Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo maana halisi ya mfarakano ambao Yesu anazungumzia katika Injili.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu kamwe hakutoa ruhusa ya matumizi ya nguvu kama njia ya kueneza Imani, bali nguvu ya Wakristo inajikita katika ukweli na upendo unaopinga matumizi ya nguvu kwani imani na vita ni mambo mawili yanayosigana kimsingi; lakini imani na nguvu ni sawa na chanda na pete kwani ni mambo yanayofumbata upole ambayo ni nguvu ya upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata kwa baadhi ya ndugu na jamaa ya Yesu walisigana kuhusu maisha na utume wake kama ambavyo yanasimulia Maandiko Matakatifu. Lakini Bikira Maria alimwelewa, akaukazia macho Moyo Mtakatifu wa Mwana wa Aliye Juu na utume wake. Ni kutokana na imani thabiti iliyoshuhudiwa na Bikira Maria, hata ndugu zake wakajikuta wakiwa ni kati ya wafuasi wa kwanza wa Yesu waliounda Jumuiya za kwanza kwanza za Wakristo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkazia macho na hatimaye kumfuasa Yesu Kristo hata pale ambapo kuna gharama kubwa, kwa kutambua kwamba, kumfuasa Yesu kunahitaji kujitosa kikamilifu kwani imani ni nguvu ya moyo na kamwe si kama urembo unaowekwa kwenye keki!

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbuka wahanga wa ajali ya Meli iliyotokea nchini Manila na hivyo kusababisha watu wengi kupoteza maisha yao. Hadi kufikia Jumapili mchana, miili ya watu 31 ilikuwa imekwishapatikana na watu wengine 170 hawajulikani waliko.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii pia kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Misri. Ametambua uwepo wa makundi mbali mbali ya waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.