Familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia
Familia zetu zinaishi katika ulimwengu, na hatuwezi kujitenga na ulimwengu huu wakati
bado tunaishi. Tunapoendelea
kutafakari mada yetu ya familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi,
sayansi na teknolojia katika mwaka huu wa imani, inafaa pia kutafakari ni jinsi gani
familia zetu zinaweza kufaidika na maendeleo haya lakini vile vile ni jinsi gani familia
zetu zinaweza kupoteza mwelekeo. Hawali ya yote inatupasa sisi wanafamilia wote
tumshukuru Mungu kwa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia. Haya ni mapendo makubwa ya
Mungu yanayoiangazia akili ya mwanadamu kutafuta njia mbadala ya kurahisisha maisha
yetu ya kila siku. Kwa mfano nikijaribu kutazama miaka ishirini iliyopita kabla
simu za mikononi au mambo ya intaneti hayajaingia katika jamii zetu nyingi, mawasiliano
yalikuwa magumu sana. Kama mtu amepata tatizo kwa mfano la msiba au natataka kuwasiliana
na familia yake, na yeye anaishi mbali na nyumbani kwake ilikuwa inachukua hata majuma
mawili kupata taarifa au kupeleka salamu. Leo hii Sayansi na Teknolojia imetuweka
karibu zaidi kwa kuweza kupata mawasiliano mara moja. Mara nyingi sisi binadamu
pale tunapofanikiwa katika maisha kwa namna yoyote kuna kishawishi cha majivuno au
kulewa mafanikio na kujiona kuwa mafanikio yote yametokana na jitihadi zetu binafsi
na kumweka Mungu pembeni. Majivuno katika mafanikio yoyote ni hatari ya kusahu mchango
wa Mungu katika mafanikio yetu. Kinyume cha majivuno ni unyenyekevu. Katika unyenyekevu
tunaalikwa kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yetu na kuelewa sisi tunabaki kuwa
binadamu ambao bila yeye hatuwezi lolote. Tukilikumbuka hilo, tutakumbuka kutoa shukrani
kwa Mungu kwa zawadi mbalimbali anazotujalia katika maisha. Tukumbuke kuwa ni
Mungu anayetujalia hekima ya kuweza kutumia maendeleo haya ya vizuri, kwa faida ya
maisha yetu na faida ndugu zetu tunao ishi nao. Hekima hii ya Mungu imefunuliwa kwetu
kupitia Maandiko Matakatifu na Mama Kanisa akiongozwa na Roho Mtakatifu amepewa jukumu
rasmi la kuendelea kufundisha ufunuo huo kwa vizazi hata vizazi “hata ukamilifu wa
dahari”(Mt. 28:20) . Bila hekima kutoka kwa Mungu, tutatumia maendeleo ya Sayansi
na Teknolojia kwa ajili kujiangamiza pamoja na familia zetu. Tukuchukulie katika mazingira
yetu ya kawaida mfano wa matumizi ya simu, mitandao, luninga nk. Vyombo hivyo ni vizuri
sana kwaajili ya maendeo ya mwanadamu, lakini vyombo hivyo visipotumika kwa busara
yaani kwa matumizi sahihi na kwa wakati sahihi huku tukizingatia maadili yetu ya Kikristo
vinaweza kusambaratisha maisha ya familia na taifa la Mungu kwa ujumla. Kwa mfano,
katika nyakati za sasa tupo tayari kutumia masaa mawili kwenye intaneti au kutazama
luninga au kuzungumza kwenye simu lakini tunaweza kukosa hata dakika kumi kwa siku
za kufanya sala za familia au kusoma neno la Mungu. Vile vile badala ya kutumia vyombo
hivi katika kueneza habari njema tunaweza kuvitumia kwaajili ya kueneza habari mbaya
zenye kutengeneza chuki na uadui katika familia zetu na jamii nzima kwa ujumla. Maendeleo
yoyote katika maisha yetu sisi binadamu yanakuwa ni hatarishi pale yanapochukua nafasi
ya Mungu na kuyafanya miungu yetu. Matokeo yake badala ya vyombo hivi kutusaidia kutujenga,
vinasaidia kutuharibu. Siku za nyuma katika maisha ya familia, kulikuwa na nafasi
ya baba na mama kukaa pamoja na kuwaeleza watoto jinsi ya kuishi maisha bora na pale
kunapotokea kasoro kurekebishana. Lakini katika wakati huu wa sasa nafasi kama hizo
zinazidi kupotea tukifikiria kuwa, familia kukaa pamoja na kufanya mazungumzo kuhusu
maisha yamepitwa na wakati. Wahenga walisema, “mali bila daftari huisha bila habari”,
maisha ya familia pia bila kufanyiwa tathmini tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda
wapi, yanaweza kutupelekea kupoteza tunu nzuri za maisha ya kifamilia. Tujaribu kujiuliza
kila mmoja wetu kwa nafasi zetu, ni wangapi kati yetu tunakuwa na muda wa kukaa na
familia zetu na kufanya tathmini ya mwelekeo wa familia kwaajili ya kuboresha maisha
yetu? Mambo hayo tunaweza kuyaona ni madogo lakini yasipo pewa kipaombele madhara
yake ni makubwa kwa siku za usoni. Sisi bibadamu mara nyingi tunapopatwa na shida
ndipo tunapoweza kumkumbuka Mungu na kumwomba atusaidie. Mungu wetu tunayemuabudu
sio Mungu wa wakati wa shida tu bali ni Mungu aliyopo wakati wote. Hivyo basi,
tumshirikishe mafanikio yetu katika Nyanja zote za maisha kwa kumshukuru, na pia tumshirikishe
yale tuliyoshindwa kuyatimiza kutokana na mapungufu yetu ya kibinadamu kwa kuomba
neema zake kusudi tujaliwe nguvu ya kuweza kuanza upya. Siku hii ya leo tumshukuru
Mungu kwa karama mbalimbali alizotujalia kwa lengo la kutaka kuifanya dunia hii sehemu
nzuri ya kuishi na tuombe hekima ya kuweza kutumia zawadi ya maendeleo ya Sayansi
na Teknolojia kwa sifa na utukufu wa Mungu. Kutoka Studio za Radio Vatican ni
mimi Padre Titus Nkane, OSB.