2013-08-19 10:28:54

Cheche za Neno la Mungu!


Paka akiondoka, Panya hutawala...

Somo la I : Waamuzi 2:11 - 19

Asiyekuwepo na lake halipo. Baada ya kifo cha Yoshua kunatengenezwa ombwe la utawala na uongozi. Waisraeli hawana tena kiongozi. Na taifa linakosa mwelekeo "there is no sense of direction". Watu wanaanza kujichanganya na malimwengu. Wanaanza hata kuabudu Mungu wa Mabaali. Wanamsahau Mungu aliyewakomboa na kuwapatia nchi ya ahadi.

Mungu anawaahidi kupata Waamuzi watakaokuwa majemedari wa vita katika sehemu mbali mbali mtawanyiko katika nchi zima ya Israeli kama vile Gideon, Samson, Debora na wengine.

Fundisho moja kwetu sisi, tujifunze kuwa hata katika nafasi za kukosa kiongozi wa kiroho kwa Misa takatifu au ibada kwa muda fulani, sisi tubaki na tabia ya kuwasiliana na Mwenyezi Mungu daima. Tuwe na sala zetu za rohoni pamoja na tafakari ya kina ya Rozari takatifu, Muhtasari makini wa Injili; Mawaridi ya sala au sala ye yote ya tafakari na Neno la Mungu. Tusiingize kisingizio cho chote cha kumuacha Mungu.

Katika somo la Injili : Mt 19:16-22, Yesu anamwambia kijana mmoja -

"nenda ukauze vitu vyote, uwape maskini na utakuwa na hazina mbinguni kisha njoo unifuate.." Tunaambiwa katika Injili kuwa kijana aliondoka kwa huzuni nyingi sana.

Leo Aug 19 tunaambiwa na Kristu mambo haya :

Katika maisha ya binadamu muda wetu ni mali sana. Jumapili iliyopita nilikuwa kwa Semina ya viongozi wa Halmashauri wa walei parokia ya Chang'ombe. Kilio cha wana semina wengi kilikuwa juu ya mahudhurio hafifu ya wana jumuiya katika vikao hasa akina baba. Kila mmoja anaweza kujisifu nina ndoa, natoa zaka, nasaidia Kanisa kwa michango.

Lakini Kristo anakuomba leo, uza muda wako ukawape maskini katika jumuiya yako. Hakuna zawadi kubwa katika maisha ya jumuiya inayowanyanyua wana jumuiya wote zaidi ya kuwa nao na kukaa nao. Zawadi ya "To be there, and to be with them" Jumuiya zetu zina watoto, maskini, walala hoi waliokata tamaa ya maisha. Uwepo wetu ni uwepo komboi "saving presence" kama nabii Isaya asemavyo "Roho wa Bwana yu juu yangu, amenipaka mafuta ili niwahubirie maskini habari njema.."(Isaya 61:1-3). Sisi tupo hivi na tunakuwa hivi kwa sababu ya jumuiya zetu (John Mbiti).

2. Tuweke mkakati na mpango wa kuuza vipaji vya akili na maarifa Parokiani. Panga programu za kufundisha hesabu, Fizikis, Kemia, au uongozi na utawala bure. Katika dunia inayotegemea kulipwa kwa vipindi vya "tuition", sisi tufanye tofauti kidogo. Tuuze na kuwapa watoto ambao wazazi wao hawawezi kutoa cho chote. Najua wengi tutanuna tukiombwa kufundisha bure kwa vile elimu ni yetu ni mali na tumeipata kwa shida. Sote tutaondoka kwa huzuni na kuwaacha watoto wakifeli na kutupa lawama zote kwa NECTA.

3. Jitihada ya kuuza utajiri wetu ni kujinyenyekeza na kujifananisha na watu wengine. Ni kujibandua na dhana kuwa utu wa mtu unatokana na kujirundikia kichuguu cha vitu vya dunia (materialism). Utu, kwa maana sahihi na pana ni tokeo la roho iliyoshiba na kutajirishwa na Mungu mwenyewe. Heri kwetu kama tu "maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.." (Mt 5:3).

4. Kuuza vyote katika maanazizi (radical view) ni kupoteza kwa muda kiasi kidogo, ila kurudishiwa mara mia kwa baraka na neema za Mungu - "tafuteni kwanza ufalme wa mbingu, mengine yote mtapewa kwa ziada.." (Mt 6:33). Kutafuta ni kukana ya kidunia, na kupewa ni kumiminiwa mibaraka kutoka mbingini.

Tusali leo kwa ajili ya mioyo yetu isitengeneze ombwe la kutokuwa na Mungu. Mungu ajaze kila sehemu ya maisha yetu. Na tuombe kuonja uchungu wa kuuza kizuri tulichonacho ili kuwainua wengine wanaotuzunguka ambao wanaokandamizwa na umaskini na ulala hoi.








All the contents on this site are copyrighted ©.