Wananchi wa Mloganzila watoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema atasimamia suala la fidia kwa wakazi
91 waliobakia kulipwa katika eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
ili liweze kuisha mwezi ujao na malipo yaandaliwe mara baada ya taratibu zote kukamilika.
Alikuwa
akizungumza katika mkutano wa dhadhura, Ijumaa, Agosti 16, 2013) uliosababishwa na
wakazi wa Mloganzila na vitongoji vyake ambao wanadai fidia ili wapishe mradi mkubwa
wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Hospitali unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa
mujibu wa ratiba yake, Waziri Mkuu alikuwa ameenda Mloganzila kukagua eneo la mradi
huo na kupata maelezo kwa watendaji kuhusu kusuasua kwa mradi huo.
Alisema
kwa utaratibu wa kawaida wa makusanyo ya Serikali, suala hilo linaweza kufanyika mwezi
Oktoba na malipo yao yataanza kupatikana Novemba mwaka huu lakini kwa vile amesikiliza
hoja zao, atafuatilia na kuhakikisha malipo hayo yanawahi kidogo.
“Kwa tarehe
ya leo, hata nifanye nini hatuwezi kuwahi kukamilisha malipo haya mwisho wa mwezi
huu (Agosti). Na hii ni kwa mujibu wa taratibu za kifedha. Nitafuatilia ili mpewe
kipaumbele katika makusanyo ya mwezi ujao,” alisema.
Kwa mujibu wa tathmini
iliyofanyika mwaka 2008 na kurudiwa mwaka 2011, wakazi hao wanatakiwa kulipwa sh.
milioni 980.6/-. Wakazi wengine 2,533 walikwishafanyiwa tathmini na kulipwa fidia
ya sh. bilioni 9.55/-.
Katika mkutano huo baadhi ya wakazi waliopewa nafasi
kuelezea kero zao, walilalamikia kuhusu viwango vidogo vya fidia walizopewa, kutolipwa
fidia kwa baadhi ya wakazi ambao walikwisha kufanyiwa tathmini, na malipo yaliyotolewa
kutolingana na ukubwa wa maeneo yao waliyokuwa wakiishi.
Akijibu hoja hizo,
Waziri Mkuu Pinda alisema chanzo cha mgogoro huo ni baadhi ya wakazi kudai walipwe
fidia ya ardhi wakati eneo hilo si lao bali lilikuwa ni mali ya kiwanda cha kusindika
nyama cha Tanganyika Packers lililokuwa likitumika kunenepesha mifugo kabla haijapelekwa
kiwandani.
“Tatizo hapa ni matumizi mabaya ya ardhi. Waliopewa eneo hawakuliendeleza,
waliliacha wazi kwa muda mrefu na tena hawakulizungushia uzio. Hali hii ilileta vishawishi
kwa watu kuanza kujipenyeza kushoto na kulia,” alisema.
Alisema anakubaliana
na madai ya wakazi 91 kutolipwa fidia zao lakini wale 2,533 lazima wakubali kwamba
tayari walikwishalipwa fidia ya maendelezo ya eneo walilokuwa wakiishi.
Akizungumzia
kuhusu mradi wa chuo na hospitali ya Mloganzila, Waziri Mkuu Pinda aliitaja mipango
ya haraka ya kuendeleza eneo hilo kuwa ni kutengeneza barabara ya kilometa 12 itakayounganisha
eneo kuu la chuo hicho. ”Huduma nyingine ambazo ni lazima zipatikane haraka ni maji
na umeme. Ili mradi uende kwa kasi, ni lazima hizi huduma zipatikane mapema,” alisema.
Aliwapongeza
wakazi hao kwa uamuzi wao wa kukubali kupisha mradi wa ujenzi wa chuo hicho uendelee
kwa vile wanatambua kwamba una maslahi kwa Taifa. ”Nimefurahi kusikia kwamba mnataka
mradi huu uendelee kwa vile mnatambua umuhimu wake,” aliongeza.
Mara baada
ya mkutano huo, Waziri Mkuu alipokea maelezo kuhusu maandalizi ya ujenzi wa mradi
huo kutoka kwa watendaji wa taasisi za Serikali kama TANROADS, TANESCO, Wizara ya
Maji, Wizara ya Elimu na Kamishna wa Ardhi.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu
alifuatana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Naibu Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid. Wengine ni Wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na
Pwani.