Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Kardinali Raymundo Damasceno Assis, Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil ili kumshukuru kwa niaba ya Familia ya Mungu
nchini Brazil kwa makaribisho makubwa waliyomwonesha wakati wa hija yake ya kichungaji
nchini Brazil, lakini kwa namna ya pekee kabisa wakati alipotembelea Madhabahu ya
Bikira Maria wa Aparecida.
Baba Mtakatifu anasema, ndani ya sakafu ya moyo
wake anahifadhi kumbu kumbu ambazo haitakuwa rahisi kufutika kwa haraka. Anaukumbuka
umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema, uliojitokeza kuhudhuria Ibada
ile pamoja na mkutano na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na Amerika ya Kusini katika
ujumla wake. Baba Mtakatifu anaendelea kumshukuru Bikira Maria wa Aparecida kwa maombezi
na tunza yake ya kimama.
Anamwomba Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil
kumfikishia salam na matashi mema kwa Familia ya Mungu nchini Brazil kwa jitihada
walizoonesha katika maandalizi na hatimaye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013 iliyofanyika mjini Rio de Janeiro. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba,
Maadhimisho haya ya Imani yatakuwa ni kipindi cha neema, baraka na mwanzo mpya kwa
Kanisa nchini Brazil.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha barua ya shukrani
kwa Kardinali Raymundo Damasceno Assis kwa kuliweka Kanisa na wananchi wote wa Brazil
chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Aparecida. Anawatakia wote baraka
zake za kitume.