Pasi na fursa za ajira, utu na heshima ya binadamu iko mashakani!
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alikazia suala la kazi na thamani ya utu na
heshima ya binadamu. Kazi ni muhimu sana katika kudumisha hadhi ya mwanadamu kwani
inampa mtu fursa ya kuweza kukidhi maisha binafsi na familia yake na hatimaye, kuchangia
katika mchakato wa maendeleo endelevu ya jamii anamoishi na kufanya kazi.
Kwa bahati
mbaya mamilioni ya vijana wa kizazi kipya yanakosa kuthaminiwa na kupewa heshima inayostahili
kwa kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa mwenyezi Mungu, kutokana na ukosefu
wa fursa za ajira,, utendaji wa kazi katika mazingira duni, dhuluma na unyanyasaji
wa wafanyakazi katika maeneo ya kazi.
Hii ni changamoto anayoigusia pia Askofu
Stephen Blaire wa jimbo la Stockton katika siku ya wafanyakazi inayoadhimishwa nchini
Marekani hapo tarehe 2 Septemba, 2013. Siku ya wafanyakazi ni wakati muafaka wa nchi
yoyote ile kuangalia na kuona jinsi inavyowajali wafanyakazi wake, anasema Askofu
Blare ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya haki na Maendeleo ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani.
Kila mwanadamu anayo haki msingi ya kuheshimiwa sio kwa sababu
ya cheo alichonacho katika jamii, bali kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wake
Mwenyezi Mungu, kama anavyosema Mtakatifu Paulo kwenye Nyaraka zake akisema: mjitahidi
katika kuoneshana wema. Tamaduni mamboleo ya watu kushindana inawalazimisha kung’ang’ania
ushindi kwa mafao binafsi, lakini Mtakatifu Paulo anatoa changamoto ya kuheshimiana,
kujenga kidugu na kuthaminiana kiutu.
Hata wakati uchumi wa nchi ya Marekani
unaonekana kuimarika, Askofu Blaire anasema bado hali ya maisha ya watu wengi hasa
maskini na wale wa kipato cha chini yanaonekana kuwa magumu zaidi kwani watu wengi
bado hawana fursa za ajira na kwamba, gharama ya maisha imepanda wakati hali ya maisha
inazidi kuporomoka.
Zaidi ya watu milioni nne hawana kazi kwa zaidi ya miezi
sita sasa, bila hata kuhesabu mamilioni ya watu ambao tayari wamekata tamaa ya kupata
kazi, kwani kwa kila nafasi ya kazi inayopatikana, huwa kuna angalau watu watano wanayoipigania.
Pengo hili la kikazi limesababisha kushuka kwa mishahara nchini humo ambapo zaidi
ya watu milioni 46, milioni kumi na sita kati yao wakiwa ni watoto, wanakumbwa na
umaskini.
Askofu Blaire anasema Kwamba, kuna uhusiano kati ya fursa za ajira,
mishahara na umaskini, kwani uchumi wa nchi hiyo hautengenezi nafasi za kutosha za
ajira ili kuwawezesha wafanyakazi kuyamudu maisha yao, na kwamba, ili kupunguza pengo
linalojionyesha kati ya watu wa kipato cha juu na maskini, kuna umuhimu wa kutengeneza
ajira muafaka, zenye kutoa mishahara ya kuwawezesha wafanyakazi na familia zao kuishi
maisha yenye heshima na hadhi ya binadamu.
Katika Waraka wake wa kichungaji
Caritas in Veritate, Upendo katika Ukweli, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita, anatoa maneno ya kinabii anaposema kwamba, tofauti kubwa za mishahara zinaongeza
tofauti hata kwenye jamii, jambo ambalo lina madhara makubwa. Hadhi ya mwanadamu
na matakwa ya haki, hasa kwa vijana wa kizazi kipya, uamuzi wa kukuza miundo ya kiuchumi
yenye maadili yatakayochangia kupunguza tofauti hizi, na kuhakikisha usalama wa kazi
kwa kila mtu ni mambo msingi.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita anasema kwamba, miundo mbinu inayoleta tofauti za kijamii sio tu inaathiri mahusiano
ya kijamii, bali pia huyumbisha hata uchumi wenyewe, ambao unachangia sehemu kubwa
ya maendeleo ya jamii husika.
Askofu Stephen Blaire anasema inasikitisha kuona
kwamba maneno ya waraka wa Gaudium et Spes (no. 63), uliotokana na Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican, miaka 50 iliyopita bado yanaonekana hata leo kwamba: wakati watu
wengine hawapati hata mahitaji msingi ya kimaisha, kuna wengine kwenye jamii hiyo
hiyo wanaoponda maisha kana kwamba hawaoni yanayowazunguka. Kwa namna hii, Jamii
inawezaje kusema kwamba, watu wanaheshimiana na kujaliana kidugu?
Ni dhahiri
kwamba, watu wengi wanatamani kuishi kwenye jamii inayosimikwa kwenye misingi ya haki
na usawa, huku kila mtu akipata fursa ya kuboresha maisha yake. Tofauti zinazoonekana
zinaweza kupunguzwa, lakini kunahitajika ujasiri katika kuendeleza mfumo unaozipunguza
tofauti hizi na kujenga zaidi usawa kwenye nyanja za ajira na kipato. Hata uwezo wa
makampuni kugawana na wafanyakazi wake sehemu ya faida inayotokana na michango yao
makini.
Pia kunahitajika mikakati maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wasio na
kazi na wale wasio na hata uwezo wa kuweza kufanya kazi. Kama familia ya Mungu, Kanisa,
jamii, mashirika ya kijamii na yale ya kibinafsi na hata serikali ina wajibu katika
kukuza heshima na hadhi ya wafanyakazi.
Vyama vya wafanyakazi vimekuwa mstari
wa mbele kusimama kidete kutetea haki za wafanyakazi na kama njia muafaka ya wafanyakazi
hao kujishughulisha kwa karibu zaidi kwenye maamuzi yanayowahusu yanayofanywa na vitengo
vyao vya kazi. Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki yamekuwa mstari wa mbele kwa kusisitiza
haki na uhuru wa wafanyakazi katika kushiriki kwenye vyama vinavyotetea masilahi yao.
Kuongezeka kwa tofauti kwenye mishahara kunaashiria tatizo moja, wafanyikazi
kutojishughulisha na vyama vinavyoshughulikia maslahi yao. Ni kweli kwamba vyama
hivi kama vyama vyovyote vile, sio vikamilifu, lakini ni muhimu kwavyo kuhakikisha
havipotezi lengo muhimu la kuhakikisha mfanyakazi anapata mishahara na faida zingine
zote anazostahili ili kumwezesha kuishi kwa heshima.
Vyama hivi pia vinapaswa
kuhakikisha kiwango cha chini cha mishahara kinapandishwa, mazingira ya kazi ni salama
kwa wafanyakazi na afya zao. Kanisa nalo liko tayari kusaidiana na vyama hivyo ili
kuhakikisha wafanyakazi wanaheshimiwa na kupewa haki zao msingi.
Mashirika
binafsi huchangia sana uchumi wa nchi na mafao ya wengi. Hata hivyo, ni kinyume na
maadili kutafuta faida kwa kuwanyanyasa wafanyakazi na kutoheshimu hadhi yao. Mashirika
haya hayana budi kujenga mshikamano unaowaheshimu wafanyakazi na wote walio pembezoni
mwa jamii, kwani uchumi wowote ule ni kwa ajili ya watu, na kwamba, hatari kubwa huingia
pale imani, utu na maadili yanapokosekana kwenye shughuli za kibiashara.
Ni
changamoto kwa Kanisa Katoliki nchini Marekani kuunga mkono mashirika yanayolinda
na kutetea maisha na heshima ya mwanadamu; kulipa mishahara ya haki na kutetea haki
msingi za wafanyakazi. Pia Kanisa linapaswa kutetea utengenezaji wa sheria zitakazowasaidia
wahamiaji nchini humo kujitokeza wazi na kuweza kufanya kazi kihalali, kwani ukosefu
wa sheria kama hizo unawafanya wahamiaji wengi kunyanyaswa, na wengine kuendeleza
shughuli kwa uficho. Ni vizuri pia kuwasaidia kupata uraia wale wanaostahili, ili
waweze nao kufaidika kihalali.
Ni vizuri kuwaheshimu wafanyakazi wahamiaji
kwani hata Marekani ilijengwa na wahamiaji waliokimbia mateso, unyanyasaji na umaskini
kwingineko, na kuelekea Marekani ili kujipatia fursa ya kutumia vipaji vyao kwa uhuru
zaidi kwa mafao yao wenyewe na ya familia zao. Kuwakaribisha wageni, wakimbizi, wahamiaji,
na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama watoto wa Mungu ni wajibu wa
kila mkriso.
Lakini, ni muhimu zaidi kudhibiti hali zote za: kisiasa, kijamii
na hata kiuchumi zinazosababisha watu kuyakimbia makazi na nchi zao. Mshikamano wa
kidugu unamaanisha kuwaheshimu wafanyakazi mahali popote pale walipo.
Askofu
Stephen Blaire anasema uchungu umezidi kwa maskini na maskini wapya wanaotokana na
mwendelezo wa mfumo wa uchumi unaokuza tofauti kwenye jamii na akawasihi watu wote
wenye mapenzi mema kusimama kidete ili kutetea haki ya kazi, mishahara ya kutosha
na kuilinda hadhi ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu.
Lengo
la maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mwaka huu nchini Marekani, iwe ni kuitikia mwito
unaotolewa kila inapohitimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwenda kuitangaza Injili ya
matumaini na mshikamano kwa wale walioathirika kwa myumbo wa uchumi kimataifa.
Imehaririwa
na Sr. Bridgita Samba Mwawasi, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.