Mikakati ya Wasalesiani wa Don Bosco katika Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu
kuzaliwa kwa Mtakatifu Don Bosco
Mheshimiwa Padre Pascual Chavez, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco anasema,
wakati huu wanapojiandaa kwa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 200 tangu alipozaliwa
Don Bosco ni mwaliko na changamoto kwa Wanashirika kuchota katika mang’amuzi ya maisha
ya kiroho ili kuweza kufanya hija ya utakatifu wa maisha mintarafu karama, maisha
na utume wa Shirika la Wadon Bosco.
Kwa mwaka
2014 wanaalikwa kwa namna ya pekee kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaobubujika
kutoka kwa historia na maisha ya Mtakatifu Don Bosco.
Tasaufi ya maisha yao
kama Shirika, inafumbatwa katika upendo wa shughuli za kichungaji unaowawajibisha
kutafuta na kuendeleza utukufu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Wanatambua
kwamba, kama Wanashirika, wanawajibishwa na upendo wa Kristo kama Maandiko Matakatifu
yasemavyo “Caritas Christi urget nos” Upendo wa Kisalesiani unajikita zaidi katika
shughuli na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wokovu wa roho za watu; hali inayojionesha
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika sekta ya elimu na majiundo ya vijana.
Wasalesiani
hawana budi kujitosa kimasomaso kutumia nguvu na karama zao kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya vijana wanaowahudumia. Lengo anasema Padre Pascual Chaves ni kuwajengea
vijana uwezo wa kuwa ni: raia wema, Wakristo hodari na raia wa maisha ya uzima wa
milele.
Ni wajibu kwa Wanashirika kutambua mambo msingi kwa maisha ya Mtakatifu
Don Bosco, shughuli na mikakati yake ya kichungaji na mbinu aliyotumia katika kuwapatia
vijana elimu, lakini zaidi, Wanashirika wajitaabishe kufahamu undani wa maisha yake
ya kiroho uliomwezesha kujenga na kuwa na mazoea mazuri na Mwenyezi Mungu katika hija
ya maisha yake. Ufahamu huu, ujikite zaidi katika tafiti makini na upembuzi yakinifu
ili hatimaye, kugundua kiini cha tasaufi ya Mtakatifu Don Bosco, inayoweza kufahamika
kwa wazazi wa vijana wanaowahudumia.
Kwa mwaka 2014, anasema Padre Pascual
Chavez, Wasalesiani watafanya tafakari kuhusu mang’amuzi ya tasaufi ya Mtakatifu Bosco;
upendo na ari ya shughuli za kichungaji na kwamba, tasaufi hii ni dira kwa miito yote.
Huu ni mwelekeo wa maisha ya Mtakatifu Don Bosco yanayopaswa kumwilishwa katika ulimwengu
mamboleo mintarafu mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Wanashirika
wa Don Bosco kwa vijana, kwa kuwasaidia kuwa na mikakati ya maisha ya ujana na miito
yao.
Padre Pascual Chavez anawataka Wasalesiani kuwa makini zaidi kwani watu
na historia imebadilika, kiasi kwamba, haishangazi siku hizi kuona hata Wakristo wenyewe
wanaishi kwa kubabaisha. Ni mwaliko kwa Wasalesiani kuwaendea na kuwashirikisha karama
na tasaufi yao vijana kutoka dini na madhehebu mengine, ili wao pia waweze kuguswa
na tasaufi ya Don Bosco.
Padre Pascual Chavez anahitimisha dhima itakayoongoza
Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Don Bosco; Awamu ya
Mwaka wa Tatu kwa kukazia: mang’amuzi ya maisha ya kiroho ya Mtakatifu Don Bosco;
dhamana ya kuishi upendo katika shughuli za kichungaji sanjari na kuwashirikisha wengine
Tasaufi ya maisha ya Wasalesiani watu wenye miito mbali mbali na kwamba, kiwe ni kipindi
cha kujisomea Maandiko ya Mtakatifu Don Bosco.