2013-08-17 11:03:44

Madaktari Wasio na Mipaka, wakunja jamvi nchini Somalia baada ya miaka 22 ya huduma!


Baada ya miaka 22 ya huduma kwa wananchi wa Somalia, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, limefunga vilago vya huduma nchini Somalia iliyoanza kunako Mwaka 1991. Uamuzi huu ni matokeo ya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya madaktari na wahudumu wa Shirika hili; utekwaji nyara, mauaji, madhulumu kiasi kwamba, utu na heshima yao kama wafanyakazi katika sekta ya afya viliwekwa rehani.

Hayo yamesemwa na Bwana Unni Karunakara, Rais wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka, alipokuwa anaelezea sababu zilizowafanya hata kuamua kufunga shughuli zao za huduma nchini Somalia. Anasema, baadhi ya wafanyakazi wa Shirika lake wamenyanyasika sana, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, wananchi wengi wa Somalia watakosa huduma msingi za afya zilizokuwa zinatolewa na Madaktari Wasiokuwa na Mipaka.

Mauaji ya wafanyakazi na utekaji nyara ni mambo ambayo Madaktari hawa wamevumilia katika kipindi chote hiki, lakini sasa wameamua kuchukua msimamo thabiti, kuwa ni onyo kwa wale wanaochezea maisha ya watu kwa mafao yao binafsi. Madktari Wasio na Mipaka walilazimika kuajiri walinzi wenye silaha ili kulinda maisha na mali zao, jambo ambalo si sehemu ya sera ya mikakati yake ya huduma.

Madaktari Wasio na Mipaka wanasema wanaweza kurudi tena nchini Somalia ili kuendelea na shughuli zao, lakini wadau wote wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanatoa fursa makini kwao ili waweze kuwahudumia wananchi wa Somalia kwa njia ya usalama, amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.