2013-08-17 09:06:56

Changamoto katika azma ya Uinjilishaji mpya!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari katika mahojiano na Radio Vatican anafafanua baadhi ya changamoto ambazo Kanisa linakabiliana nazo katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa sasa. RealAudioMP3

Utandawazi na athari zake ni kati ya changamoto kubwa zinazolikabili waamini wengi, lakini hasa zaidi wale wanaotoka kwenye nchi ambazo zilibahatika kusikia kwanza Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa kwao, lakini sasa wamekengeuka kiasi kwamba, wanataka kumn'goa Mwenyezi Mungu kutoka katika maisha na vipaumbele vyao. Huu ni mwanzo wa kuporomoka kwa misingi bora ya maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Uinjilishaji mpya ni mwaliko kwa waamini kumpatia Kristo kipaumbele cha kwanza katika maisha yao ya kila siku.

Askofu mkuu Rugambwa anaendelea kusema kwamba, Nchi zile ambazo zilikuwa na Mapokeo na Utamaduni wa Kikristo, zikawa mstari wa mbele kutuma idadi kubwa ya Wamissionari kwenda sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo, leo hii zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa Wahudumu wa Injili. Hii ni changamoto kwa Makanisa ya zamani kushirikiana kwa hali na mali na Makanisa ya Kimissionari katika mikakati ya kichungaji, ili kusaidia kupunguza uhaba wa wachungaji unaoendelea kujitokeza hasa katika nchi za Ulaya.

Ukata wa fedha kwa ajili ya kugharimia mchakato wa Uinjilishaji ni kati ya changamoto ambazo zinajitokeza kwa sasa. Askofu mkuu Protase Rugambwa anasema, Mashirika ya Kipapa ya kazi za Kimissionari yana jukumu la kumsaidia Baba Mtakatifu kutekeleza wajibu wake barabara ndani ya Kanisa. Mashirika haya yamekabidhiwa dhamana ya kuhamasisha, kukuza imani na kumtangaza Kristo katika medani mbali mbali za maisha.

Hili ni jukumu ambalo linawashirikisha waamini na watu wote ili kuweza kuchangia kwa hali na mali. Takwimu za miaka kumi iliyopita zinaonesha kwamba, mchango wa raslimali fedha kutoka kwa waamini kwa ajili ya kugharimia shughuli za Uinjilishaji umepungua kwa kiasi kikubwa. Mwelekeo huu kwa kiasi kikubwa unachangiwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Hizi ni baadhi ya changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi ili mchakato wa Uinjilishaji uendelee kushika kasi katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.