Ajali ya meli yasababisha maafa makubwa nchini Ufilippini
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Askofu mkuu Jose S. Palma
wa Jimbo kuu la Cebu nchini Ufilippini kufuatia ajali ya Meli ya Abiria iliyokuwa
imebeba abiria 841 na kati yao 600 wameokolewa baada ya Meli ya abiria kugonga na
Meli ya mizigo iliyokuwa inaingia bandarini usiku wa kuamkia, Jumamosi, tarehe 17
Agosti 2013. Watu 200 hawajulikani waliko na baadhi ya miili imekwishapatikana.
Ujumbe
wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu
mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu anawaombea abiria wote waliopoteza maisha yao pumziko
la milele na kwa majeruhi kupata nafuu ili hatimaye, waweze kuendelea na shughuli
zao za kila siku. Baba Mtakatifu anapenda kuwafariji wote walioguswa na maafa haya
kwa njia ya sala na sadaka yake.