Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 20 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Mpendwa ninakukaribisheni katika safari ya tafakari Neno la uzima kadiri tulivyojaliwa
na Mama Kanisa. Leo tunasafiri pamoja katika Dominika ya 20 ya Mwaka C wa Kanisa.
Ujumbe wa
furaha na wa kukujalia maisha ni kwamba, Bwana amekuja kuleta moto duniani. Moto huo
ni Roho Mtakatifu. Tunaanza kufikiria maramoja zawadi ya Pentekoste. Hivi kama moto
huo usingetupwa duniani, Kanisa lingekuwaje sasa, Bwana ajua lakini lingekuwa pengine
limezimika, bila maisha, bila maisha ya mbele! Moto wa Injili kama nilivyokwisha ni
Roho wa Mungu, ni mapendo ya Mungu, ni maisha hai.
Mpendwa, kama Injili inaadhimisha
huo moto wa upendo basi kwa vyovyote vile maisha hayawezi kutafsiriwa kama maisha
ya kujifurahisha bali maisha ya huduma kwa waliowahitaji.
Ndiyo kusema, tunapata
ujumbe huo katika maneno ya Bwana mwenyewe sikuja kuwafanya mkakae kwa amani bali
nimekuja kuwatingisha na kuwashitua ili mkawajibike katika kujenga maisha ya kumwelekea
Mungu.
Bwana anaendelea katika Injili kutoa maneno mazito ambayo tusipokuwa
waangalifu twaweza kupotea. Anasema nimkuja kuleta utengano na mafarakano. Katika
hali ya kawaida kuna utengano kulingana na itikadi, rangi, umri nk. Bwana hazungumzii
hayo bali ataka kutufundisha kuwa ulimwengu huu haundeshwi kwa mantiki tu ya kibinadamu
bali kwa moto wa Pentekoste, moto wa Injili ambao huzigonga dhamiri zetu. Moto ambao
huwasha mapendo ya mioyo yetu ili yaweze kuendana na safari ya wokovu ambayo hujitokeza
kwa njia ya Jumuiya. Moto huu hutaka tufikirie juu ya mambo ya uzima wa milele badala
ya kufikiria mambo ya kawaida.
Mpendwa msikilizaji wa radio Vatican, kama moto
huu ukikolea katika maisha ya watu basi huweza pia kufika katika familia zetu na kuwasha
mwanga ambao waweza kujenga utengano kwa namna moja au nyingine. Katika Kanisa, Jumuiya
ya waamini wapo ambao wameupokea moto huo moja kwa moja na hivi wanakuwa chanzo cha
maisha ya kujitoa kikamilifu kwa ajili ya wengine. Hali hii yaweza kuzaa kutoelewana
na hasa kwa wale wasio na imani. Hata hivyo yatupasa kutambua kuwa Upendo ambao ndio
moto unaotupwa duniani huvumilia na kuyaona yote katika jicho la Bwana kadiri ya Mtakatifu
Paulo.
Barua kwa Waebrania yatufundisha kusadiki kina na kuvumilia mateso yatakayotoka
na moto uliotupwa duniani na Bwana. Mfano wa uvumilivu ni watakatifu, wafiadini na
hasa Bwana wetu Yesu Kristo aliyekubali kuteswa hadi kufa Msalabani. Jambo hili linampata
Yeremia katika Somo la Kwanza anapotumwa kuwaambia Wayahudi kuwa mji wa Yerusalemu
utatekwa, basi wakuu wanachukia na kukamata na kumtupa katika shimo kuu. Kwa huruma
ya Mungu anaokolewa katika taabu hiyo. Basi nasi katika kuishi imani yetu kwa hakika
kutakuwa na taabu ambazo tunahitaji kuzivumilia.
Baba Mtakatifu Francisko
anasema, pengine nyakati hizi kuna mashahidi na waungama dini wengi wanaoendelea kutoa
maisha yao kwa ajili ya ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake, kuliko wakati ule wa Kanisa
la Mwanzo.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii inaletwa kwako na Padre
Richard Tiganya, C.PP.S.