2013-08-16 08:43:16

Salini kwa ajili ya amani, majadiliano na upatanisho wa kitaifa nchini Misri!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho kama Kanisa linavyofundisha na kusadiki, aliwaalika waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema kuungana naye kwa ajili ya kusali na kuwaombea waathirika wa machafuko ya kisiasa nchini Misri.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Libertà ulioko mjini Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, siku ya Alhamisi, tarehe 15 Agosti 2013.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote walioguswa na machafuko hayo ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao ya ndani.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani, majadiliano ya kina sanjari na upatanisho wa kitaifa nchini Misri na kwenye maeneo ambayo damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika.

Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria Malkia wa amani kuiombea dunia iweze kuwa ni mahali pa amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Katika kipindi hiki cha machafuko huko nchini Misri zaidi ya Makanisa 20 yamechomwa moto katika Majimbo kadhaa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wenye misimamo mikali ya kidini. Baadhi ya wananchi wenye mapenzi mema waliwazuia vijana waliokuwa wanataka kuchoma moto nyumba ya Watawa, wamezuiwa na wananchi wenye mapenzi mema kwa kusema kwamba, kwa miaka 70 Watawa hao wamekuwa wakitoa huduma safi kwa wananchi wa Assiut, nchini Misri, kwa msimamo huu, nyumba ya watawa ikasalimika!All the contents on this site are copyrighted ©.