Miaka 110 ya kuzaliwa kwa mtetezi wa wagonjwa wa ukoma duniani!
Jumuiya ya kimataifa tarehe 17, Agosti 2013 inaadhimisha siku ya 110 ya kuzaliwa kwa
mtume wa waathirika wa ugonjwa wa ukoma Raoul Follereau aliyezaliwa Nevers, Ufaransa
tarehe 17 Agosti 1903 na kuaga dunia mjini Paris, Ufaransa, tarehe 6 Desemba, 1977.
Raoul alikuwa
ni mwanzilishi wa chama cha Raoul Follereau ambacho kinasaidia na kuwatetea waathirika
na wagonjwa wa ukoma, na hasa kwenye nchi za kiafrika. Mtazamo wa Kikristo uliomwezesha
Follereau kufanya kazi hii na nyinginezo kwa mapendo ulikuwa chanzo cha kuanzishwa
maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wagonjwa wa Ukoma iliyofanyika kwa mara ya kwanza
Januari 1954.
Ili kumkumbuka mtume huyu wa waathirika wa ukoma, Jumuiya ya
kimataifa imeandaa namna mbalimbali za kuadhimisha Siku hii kwa mwaka 2013. Ramsha
ramsha hizo zitafanyika nchini Ufaransa na kwingineko duniani, mojawapo ikiwa ni kutolewa
kwa stempu ya kipekee na Kitengo cha Posta cha Mji wa Vatican.
Mtume Raoul
Follereau alizaliwa huko Nevers, Ufaransa mnamo 1903. Akiwa bado kijana mdogo alipata
kuvuma kwenye magazeti ya Ufaransa kama mwandishi wa habari na mtunzi stadi wa mashairi.
Katika moja ya safari zake Barani Afrika kama mwandishi wa habari, akiandika juu ya
maisha na huduma za Padre Charles De Foucauld kwenye maandalizi ya maadhimisho ya
miaka 20 tangu kifo cha Padre huyo, kijana Raoul Follereau alikumbana ana kwa ana
na waathirika wa ugonjwa wa ukoma.
Tukio hili lilimgusa sana rohoni na akilini
mwake na hivyo kubadili maisha yake moja kwa moja kadiri ya mwanga wa imani. Huu ukawa
ndio mwanzo wa safari yake ya kuwahudumia na kutetea haki za waathirika wa ugonjwa
wa ukoma, akisaidiana na mkewe Madelaine Boudou.
Kwa miaka kumi iliyofuata
Raoul Follereau aliizunguka dunia akiongoza mikutano na semina zaidi ya elfu moja
ambayo ilimsaidia kuchangisha fedha za kuanzisha Hospitali ya waathiriwa wa ukoma
mjini Adzope, nchini Ivory Coast. Leo hii Hospitali hiyo inajulikani kama Taasisi
ya Kitaifa ya Kutibu Ukoma R. Follereau.
Hata hivyo, Raoul Follereau hakuridhika
na kuwa tu na Hospitali kwa ajili ya matibabu, msukumo wa mapendo kutoka ndani ya
roho yake ulimtaka pia kuhakikisha kuwa waathirika wa ugonjwa wa Ukoma hawabaguliwi
wala kutengwa na jamii kama ilivyokuwa ikitokea, jambo ambalo liliwakosesha furaha
wagonjwa hao kwani hawakujitakia ugonjwa huo.
Alitumia uwezo wake kama Mwandishi
kuandika juu ya ugonjwa wa Ukoma na kulijulisha Shirika la Afya Duniani kwamba, ukoma
ni ugonjwa kama ugonjwa wowote ule wa kuambukiza, ulikuwa na tiba, sio ugonjwa wa
kurithi, na kwamba haikuwa vyema kuwatenga waathiriwa wa ugonjwa huo.
Tarehe
20 mwezi Septemba 1952, Raoul Follereau aliuomba Umoja wa Mataifa kuanzisha mkataba
ambao ungeweka wazi sheria kuhusiana na ugonjwa wa ukoma na kuhakikisha ulinzi wa
haki za waathirika na kuwatoa kwenye jela ya kihisia walimokuwa wamefungwa kwa kutengwa
na jamii. Ombi hili lilikubalika hapo 1954, miaka miwili baadaye, kwenye kikao cha
kitaifa cha Ufaransa. Ni katika mwaka huu pia ambapo Umoja wa Mataifa ulianzisha
Siku ya Ugonjwa wa Ukoma Kimataifa.
Lengo ni kuhakikisha kwamba, waathirika,
sawa na wagonjwa wengine wote, wanapata fursa ya kutibiwa na kuheshimiwa kama binadamu.
Zaidi ya hilo, alikuwa pia na lengo la kuiponya jamii kutokana na woga kuhusu ugonjwa
wa ukoma uliojiri sana nyakati hizo sehemu mbali mbali za dunia.
Leo hii
siku hii inaadhimishwa na zaidi ya mataifa 150 kote duniani; ni maadhimisho yanayoashiria
kukamilika kwa lengo la mwanzilishi wa siku yenyewe, ambaye alitamani sana kuona mshikamano
wa kimapendo na furaha kwa wagonjwa wote wanapochukuliwa kama binadamu, kitu ambacho
ni cha kujivunia, kwani thamani yake ni kubwa zaidi kuliko misaada yoyote ile inayoweza
kutolewa.
Jumuiya ya kimataifa inapoadhimisha miaka 110 ya kuzaliwa kwake mtume
huyu wa Waathirika wa Ugonjwa wa ukoma inajivunia mchango wake uliotokana na bidii,
ujasiri, na msukumo wa upendo wa Kikristo. Ni changamoto kwao wakristu wa kizazi
kipya kuitunza tunu hii inayojidhihirisha pale Yesu Kristo mwenyewe alipoyatoa maisha
yake na kufa msalabani kwa ajili ya nduguze.
Leo hii kuna vyama na mashirika
yaliyoenea kote duniani kumuenzi Raoul, na kuendeleza huduma kwa maskini na wale waliosukumizwa
pembezoni mwa jamii. Vyama hivi ni kama kile cha Marafiki wa Raoul chenye matawi
kama vile Italia, India na Ufaransa. Marafiki wa Raoul Follereau pia wako katika
nchi kadhaa za kiafrika kama vile Msumbiji, Ivory Coast, Togo, Congo, Sudan, Rwanda,
Burundi, Tanzania na Angola.
Wakati wa uhai wake, Raoul Follereau alipata,
kuandika vitabu kadhaa juu ya mapendo kama vile: “Bila Wewe Hakuna Mapendo; Fanya
Maisha yetu yang’ae Upendo; na zaidi alimwomba Mungu kuwaponya binadamu na ukoma wa
kweli ambao ni kumsulubu Yesu kwa kutowajali ndugu zake waathirika wa ugonjwa wa Ukoma.
Ni mfano kwa wote wale wanaopania kumfuata Yesu Kristo kwa vitendo sanjari na kujitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya wengi.
Makala hii imeandaliwa
na Sr. Bridgida Samba Mwawasi, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.