2013-08-16 07:49:18

Maaskofu wa Majimbo yaliyoko kwenye Visiwa vya Bahari ya Hindi wakutana Madagascar


Hivi karibuni, Wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki katika Visiwa Vilivyoko Bahari ya Hindi (CEDOI) walikutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, (CEM) ili kubadilishana mawazo, uzoefu na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kwa mara ya kwanza Maaskofu wa Mabaraza haya mawili wameweza kukutana. RealAudioMP3

Taarifa ya mkutano huo inabainisha kwamba, Maaskofu waliweza kuangalia kwa pamoja mikakati ya shughuli za kichungaji katika sekta ya elimu, maisha na ndoa mintarafu mazingira na tamaduni za wananchi wanaoishi katika Visiwa vilivyoko kwenye Bahari ya Hindi. Wameangalia kwa pamoja changamoto, matatizo na fursa zilizopo katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene katika nchi zao.

Wanasema, wamegusia pia mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakaowasaidia wageni wahamiaji kuweza kupata huduma za Kikanisa. Ilikuwa ni nafasi kwa Maaskofu kuweza kujadiliana pia masuala ya shughuli za kimissionari kama sehemu ya changamoto ya Mama Kanisa katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Mwelekeo huu unahitaji mshikamano wa kimissionari na umoja wa Kanisa ili kufanikisha azma hii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; ulimwengu unaoonesha kila dalili za ukanimungu, lakini bado kuna watu wana kiu na njaa ya kutakana kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Maaskofu hawa wameamua kukutana mara kwa mara ili kuimarisha mshikamano wao katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa. Hapo mwakani, 2014, Maaskofu kutoka katika Visiwa vilivyoko kwenye Bahari ya Hindi watakutana nchini Mauritius.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka, ambao umepembua hali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiroho nchini humo. Maaskofu wanaendelea kuwaalika waamini na wananchi wenye mapenzi mema nchini Madagascar kusali kwa ajili ya haki, amani na upatanisho.

Kuhusu hali ya maisha na utume wa Kanisa nchini Madagascar, Maaskofu wamezungumzia kuhusu: hali ya miito, Seminari na changamoto zake pamoja na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya waamini walei, ili waweze kujikita katika maisha na utume wa Kanisa, wakitambua dhamana yao ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar linatarajia kukutana tena hapo Novemba, 2013.
All the contents on this site are copyrighted ©.