2013-08-16 09:05:16

Hali ni tete nchini Misri!


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anaungana na viongozi wengine kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kulaani mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kupamba moto nchini Misri. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea mchakato wa uponyaji, haki na amani miongoni mwa wananchi wote wa Misri.

Ni jambo la msingi ikiwa kama wananchi wote wa Misri watakuwa na haki sawa na dhamana pamoja na wajibu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi. Wananchi wa Misri wakubali tofauti zao za kisiasa na kidini kama changamoto ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasikitishwa sana na wimbi la uchomaji wa Makanisa unaofanywa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kiimani.

Kuanzia mwaka 2011 Misri imeendelea kukabiliana na machafuko ya kijamii hali ambayo bado inaendelea kusababisha maafa makubwa. Umefika wakati kwa wananchi wa Misri kusahau tofauti zao za kisiasa na kidini na kuanza kutafuta misingi ya haki, amani na upatanisho; ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza mbele yao. Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, vita inayoendelea nchini Misri haitatafsiriwa kuwa ni vita kati ya Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo. Viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanaendelea kuungana na watu wenye mapenzi mema kwa ajili ya kuombea amani na utulivu.

Taarifa ya Wizara ya Afya inaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2013, zaidi ya wananchi 623 wamekwishapoteza maisha kutokana na mashambulizi yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali nchini Misri. Pengine idadi hii ikaongezeka maradufu.

Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wamelaani mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yanayoendelea nchini Misri. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amelaani matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi dhidi ya raia. Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ina wajibu wa kuhakikisha kwamba, inajitahidi kuzuia ili Misri isitumbukie katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo itasababisha maafa makubwa!All the contents on this site are copyrighted ©.