Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria inatoa matumaini, lakini vuteni subira!
Shirika la Afya Duniani, WHO limepokea kwa mikono miwili taarifa iliyotolewa hivi
karibuni na watafiti wa ugonjwa wa Malaria kutoka Marekani kwamba, wamefanikiwa kupata
chanjo dhidi ya wadudu wa Malaria. Hii ni habari inayotia matumaini kwa mamillioni
ya watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Malaria hasa Barani
Afrika. Chanjo hii ambayo
kwa sasa imepewa jina Pfspz imefanyiwa utafiti na majaribio huko Maryland, Marekani
na kuonesha mafanikio makubwa, lakini watu waliofanyiwa majaribio ya chanjo hii walikuwa
ni wachache, ndiyo maana Shirika la Afya Duniani linawataka watu kuvuta subira wakati
ambapo juhudi zinaendelea kubainisha juu ya ufanisi wa chanjo hii. Shirika la
Afya Duniani linasema kwamba, hadi sasa kuna chanjo 20 ambazo zimefanyiwa utafiti
katika hatua mbali mbali kabla ya kuthibitisha kwamba, zinafaa kwa ajili ya matumizi
ya chanjo dhidi ya Malaria kwa umma mkubwa zaidi. Takwimu za Shirika la Afya Duniani
kwa Mwaka 2010 zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 660,000 wamefariki dunia kutokana
na ugonjwa wa Malaria. Waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Malaria Barani Afrika ni watoto
wenye umri chini ya miaka mitano.