2013-08-16 08:12:37

Baada ya miaka 22 ya sadaka na majitoleo, waamini wakamilisha ujenzi wa Kanisa!


Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti 2013 sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Burkina Faso, Kanisa la Bikira Maria Mama Yetu wa Yagma, limetangazwa kuwa ni Kanisa kuu dogo.

Hayo yamesemwa na Abate Narcisse Guigma, msimamizi mkuu wa Kanisa kuu dogo la Bikira Maria Mama Yetu wa Yagma, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni ambayo kwa Mwaka 2013 yameongozwa na kauli mbiu "Pamoja na Bikira Maria, mfano bora wa imani, tumshukuru Mungu aliyewainua wanyonge kutoka mavumbini".

Kanisa hili limejengwa kwa mfano wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa, ili kutoa heshima kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Jiwe la msingi wa ujenzi wa Kanisa hili liliwekwa kunako mwaka 1978. Kutokana na sababu mbali mbali ujenzi huu ulicheleweshwa. Kunako Mwaka 1991 wakati wa hija ya kichungaji ya Mwenyeheri Yohane Paulo II nchini Burkina Faso, ujenzi wa Kanisa hili ukaanza kushika kasi. Kunako Mwaka 1998, Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso likatangaza kwamba, Kanisa la Bikira Maria Mama Yetu wa Yagma kuwa ni Madhabahu ya hija za kitaifa.

Ujenzi wa Kanisa hili umedumu takribani miaka 22, lakini waamini hawakukata tamaa, bali waliendelea kuwa na imani na matumaini kwamba, iko siku wangeweza kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Mradi huu mkubwa umegharimiwa kwa asilimia 85% na mchango wa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Burkina Faso. Waamini wakiamua kulitegemeza Kanisa wanaweza.

Kila mwaka, Mwezi Februari ni kipindi cha hija za waamini kutoka Majimbo mbali mbali wanaokwenda kutoa heshima kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Waamini kutoka nchi jirani wanahudhuria pia, kilelezo cha mshikamano wa imani katika hija ya maisha ya Wakristo.All the contents on this site are copyrighted ©.