2013-08-15 08:11:02

Vijana jitoseni kimasomaso kuijenga nyumba ya Mungu!


Inasemekana kwamba wito wa Mtakatifu Francisko wa Assisi ulianza pale alipoisikia sauti ikimwambia: “enenda ukaijenge upya nyumba yangu”. Sauti hii ilitoka kwenye Msalaba Mtakatifu uliokuwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Damiani; wakati alipokuwa akisali. RealAudioMP3

Maneno hayo yalitumiwa kwenye mchezo wa kuigiza na kundi moja la vijana katika sherehe za kufungua Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani iliyofanyika Rio di Janeiro Brazil, na hivyo kumpa Baba Mtakatifu Francisko mada ya tafakari yake ya kwanza kwenye maadhimisho hayo. Anasema kijana Francisko aliitikia kwa ari mwito wa kuijenga nyumba ya Bwana, japo kwa wakati huo hakuelewa vizuri ni nyumba ipi aliyokuwa anatumwa kuijenga.

Hatimaye, Kijana Francisko aliyekuwa ni moto wa kuotea mbali enzi ya ujana wake, alielewa kwamba, halikuwa ni suala la kuijenga nyumba ya udongo na matofali, bali kutoa mchango wake kwenye ujenzi wa maisha ya Kanisa la Mungu: akilihudumia, kulipenda na kumfanya Kristo ang’ae zaidi ndani ya Kanisa hilo kwa njia ya huduma makini kwa Mungu na jirani.

Ni tafakari ya kina inayotolewa na Askofu mkuu Bruno Forte wa Jimbo kuu la Chieti-Vasto, Italia wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kutafakari yale yaliyojiri kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Brazil.

Anasema, Mwanga huu ulionekana wazi pale Baba Mtakatifu Francisko aliposimama mbele ya mamilioni ya vijana mjini Rio na kuwataka kujihusisha zaidi na maisha ya Kanisa kwa kuwa mstari wa mbele, na sio tu kama watazamaji bali wadau na vyombo makini kwenye ujenzi wa dunia mpya na Kanisa jipya; Kanisa changa na zuri zaidi. Aliwataka vijana kufanya uamuzi binafsi na kujitolea zaidi katika kujenga haki na usawa kwa ajili ya mafao ya binadamu wote, kulingana na mpango wa Mungu.

Aliwataka vijana kutokata tamaa kutokana na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo, bali waendelee kuwa ni watu wa matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Papa Francisko anawahimiza vijana kuwa makini katika kuisikiliza sauti ya Mungu kwani katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna sauti na walimu uchwara wanaoendelea kupaaza sauti yao kila kukicha!

Ni kipindi cha kumwachia Kristo na Kanisa lake aweze kuingia katika sakafu ya mioyo ya vijana, akue na kupata maskani ya kudumu, matokeo yake ni kuwawezesha vijana hawa kuwa kweli ni mashahidi wa Injili na wadau wa Uinjilishaji miongoni mwa vijana wenzao sehemu mbali mbali za dunia.

Vijana waliguswa hasa pale Baba Mtakatifu alivyoongelea juu ya maisha yake kama mwanamichezo ambaye yumo hata kama havumi! Akaonesha umuhimu wa kufanya mazoezi ili kuweza kupata tuzo analowania. Vijana kama wanamichezo wa Kristo wanayo fursa na uwanja mpana zaidi wa kuweza kushirikisha karama na vipaji vyao katika maisha na utume wa Kanisa, ili hatimaye, waweze kupata furaha ya maisha ya uzima wa milele.

Vijana waendelee kujibidisha katika Sala, tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti pamoja na matendo ya huruma kwa jirani wanaokutana nao katika hija ya maisha. Anasema, hizi ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za maisha ya ujana ambao wakati mwingine ni nongwa kwa ambavyo wamewahi kusema baadhi ya viongozi wa Kanisa.

Vijana wakumbuke kwamba hawapo peke yao kwenye kinyang’anyiro hiki, bali wanayo Jumuiya nzima ya waamini na kwamba, maisha ya sadaka ni ya lazima, lakini yanarahisishwa kwa kutambua kwamba ni hii ni safari ya Familia ya Mungu na wala siyo ya mtu binafsi. Kila mmoja anao mchango wake binafsi kwenye Jumuiya hiyo na hivyo vijana wasikubali kushika mkia katika kutimiza wajibu wao ndani ya Kanisa, bali hata wao wajisikie huru kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani.

Askofu mkuu Bruno Forte wa Jimbo kuu la Chieti-Vasto, anasema Papa Francisko anaendelea kuwashangaza wengi hasa kutokana na utumiaji wa lugha rahisi inayoeleweka na waamini moja kwa moja. Anaendelea kuwahusisha vijana na waamini kwa ujumla katika ujenzi wa Kanisa la Kristo. Kwa hakika ni: Papa mnyenyekevu; mwenye huruma; mpenda watu! Ni Papa wa vijana, kama ilivyojidhihirisha kwenye maadhimisho ya Rio De Janeiro, nchini Brazil.

Imehaririwa kutoka Gazeti la L’Osservatore Romano
Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.