2013-08-15 12:08:50

Bikira Maria ni kielelezo cha utu na wito wa wanawake wote!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, aliwaalika waamini na mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Libertà mjini Castel Gandolfo, kusali kwa pamoja ile sala ya Malaika wa Bwana, iliyomwezesha Bikira Maria kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Jibu la "Ndiyo" kutoka kwa Bikira Maria ulikuwa ni mwanzo wa safari yake kwenda kwenye maisha ya uzima wa milele. Haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwamba, kila mtu aweze kuwa na maisha tele, na kwamba, wote wanakabirishwa nyumbani kwa Baba.

Baba Mtakatifu Francisko, ametumia fursa hii kukumbuka Miaka 25 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa Kichungaji kuhusu utu na wito mwanamke, "Mulieris Dignitatem". Waraka huu una utajiri mkubwa unaopaswa kufanyiwa tafakari ya kina, kwani unagusa kwa namna ya pekee maisha ya Bikira Maria.

Ni Waraka uliotolewa wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la maisha ya Mwanamke mintarafu Maandiko Matakatifu na kwamba, wanawake wote kwa mfano wa Bikira Maria waweze kujisikia utimilifu wa wito wao.

Baada ya Maadhimisho yote haya, Baba Mtakatifu Francisko alipata fursa ya kutembelea Parokia ya San Tommaso da Villanova, iliyopo mjini Castel Gandolfo na baadaye alirejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha yake ya kawaida.All the contents on this site are copyrighted ©.