2013-08-15 11:19:33

Bikira Maria ana nafasi ya pekee katika maisha na utume wa watawa!


Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa anayo nafasi ya pekee katika maisha ya wanawake, lakini zaidi kwa watawa wanaojitoa kimaso maso kwa ajili ya kumpokea, kumpeleka na kumshuhudia Kristo kati ya Mataifa. Wanawake pia wana dhamana kubwa katika kulinda, kutetea na kulea zawadi ya maisha kama alivyofanya Bikira Maria katika Fumbo la Umwilisho. RealAudioMP3

Kwa waamini wote katika ujumla wao, wakumbuke kwamba, wamepewa zawadi ya imani wanayopaswa pia kuilinda, kuikuza na kuitolea ushuhuda pamoja na kuwashirikisha wengine kama alivyofanya Bikira Maria katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Ni maneno ya Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu wakati wa mahojiano na Radio Vatican kuhusu nafasi ya Bikira Maria katika maisha ya waamini na changamoto ya ushuhuda wa imani hiyo, kama kielelezo cha ukomavu wa maisha na wito wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Bikira Maria mara baada ya kupokea wito wa kuwa ni Mama wa Mungu, aliendelea kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, kamwe hakukata tamaa alipokumbana na vizingiti katika hija ya maisha yake. Hii ni shule tosha kabisa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiendelea kumjifunza Kristo kwa njia ya shule ya Bikira Maria, kila mtu kadiri ya maisha na wito wake ndani ya Kanisa.

Waamini waendelee kuboresha miito yao ili wawe kweli nimifano bora ya kuigwa na wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Kwa njia hii wanashiriki katika utekelezaji wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe.

Sr. Maria Eugenia Thomas anasema kwamba, Bikira Maria alitambua alitambua kwamba utume wake ulikuwa ni mgumu na wenye kuwajibisha, ndiyo maana aliamua kumrudishia Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa utenzi wa "Magnificat". Hii ina maana kwamba, kila mwamini na kila mtu anayo nafasi ya kuchangia mchakato wa maboresho ya maisha ya wengi kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu; daima wakijitahidi kujenga mshikamano wa upendo unaojikita katika kanuni ya auni.

Kila mtu ajitahidi kuwa ni chombo cha amani na upatanisho kati ya Mungu na jirani; na kati ya mwanadamu na mazingira yake; daima wakisukumwa kutafuta mafao ya wengi. Waamini wajifunze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo pamoja na kuambatana naye katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini wajifunze kutembea pamoja kama Jumuiya, kwa kuanzia katika familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Parokia, Jimbo na mshikamano huu ujioneshe pia katika Kanisa la Kiulimwengu.

Waamini wataweza kuyatakatifuza malimwengu ikiwa kama watayajenga maisha yao katika Sala, Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa njia ya matendo ya huruma, yaani huu ndio mwelekeo wa imani katika matendo kwa ajili ya kuinua utu na heshima ya binadamu anayetanga tanga katika shida na mahangaiko ya ndani.All the contents on this site are copyrighted ©.