2013-08-14 11:40:51

Wagawieni watu Mafumbo ya Kanisa kwa imani na uchaji mkuu!


Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa Mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati; hivyo hii ni Sakramenti ya huduma ya kitume nayo ina ngazi kuu tatu: yaani Uaskofu, Upadre na Ushemasi.

Mapadre kwa mamlaka wanayokabidhiwa na Mama Kanisa wanakuwa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa katika maeneo yao. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Hutenda kwa nafsi ya Kristo na kutangaza Fumbo lake; huyaunganisha maombi ya waamini na Sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa kila siku katika Ibada ya Misa Takatifu. Ni daraja linalowataka kujenga na kuimarisha umoja kati yao kama Mapadre pamoja na Askofu wao.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo kwa kupewa chapa isiyofutika na hivyo kufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi na Mhudumu wa wote. Shemasi ni msaidizi mkuu wa Askofu na Mapadre katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Ni wahudumu wa Neno la Mungu na matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Hivi karibuni Askofu mkuu Cyprian Lwanga wa Jimbo Kuu la Kampala Uganda, alitoa Daraja takatifu la Upadre kwa Mashemasi 4; Daraja la Ushemasi kwa Majandokasisi 3 pamoja na Nadhiri kwa Mabruda 3 wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko, lililoanza kutekeleza utume wake nchini Uganda kunako Mwaka 1988.

Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Madhabahu ya Padre Pio, huko Kabulamuliro, Wilani Akiso, Uganda, Askofu mkuu Lwanga alisema kwamba, Mapadre wamepewa dhamana ya kuwaondolea waamini dhambi zao kama njia ya kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajipatanisha na Mungu kabla ya kujongea na kushiriki Altare ya Bwana.

Sakramenti ya Upatanisho inamwandaa mwamini kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti hii. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inamkirimia mwamini nguvu na neema za kuweza kumwilisha kweli za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao.

Askofu Lwanga anawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, wanawapatia waamini nafasi ya kujipatanisha na Mungu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.All the contents on this site are copyrighted ©.