Waamini wanamsubiri Papa Francisko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo kwa Ibada ya Misa,
tarehe 15 Agosti 2013
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho inayoadhimishwa
na Mama Kanisa kila Mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa
kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, iliyoko
nje kidogo ya mji wa Roma. Mara baada ya Misa, Baba Mtakatifu atasali Sala ya Malaika
wa Bwana, na waamini pamoja na mahujaji watakaokuwa wamefika mjini Castel Gandolfo.
Kabla
ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko anatarajiwa kuwatembelea
Watawa wa ndani wa Mtakatifu Klara wanaoishi hapo mjini Castel Gandolfo. Hii ni Monasteri
iliyojengwa kunako mwaka 1631. Ikabomolewa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, hali
ambayo iliwalazimisha Watawa waliokuwa wanaishi kwenye Monasteri hii kuhamishiwa mjini
Roma.
Katika kipindi hiki, Kanisa kwa namna ya pekee linamkumbuka Marehemu
Sr. Maria Chiara Damato aliyefarkki dunia hapo tarehe 9 Machi 1948 kwa ugonjwa wa
Kifua Kikuu. Tayari mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri unaendelea baada ya mwili
wake kufukuliwa kunalo tarehe 22 Novemba 1999 na kukutwa bado haujaharibika.
Watawa
wanaoishi kwenye Monasteri hii wanautumia muda wao mwingi kwa ajili ya: Sala, Tafakari
na Kazi. Wanawasaidia waamini katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, katika Kikanisa
ambacho kiko wazi kwa ajili ya wageni kutoka nje. Ni watawa ambao wamebobea katika
kazi za mikono na matunda ya kazi za mikono yao wanagawana na maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kadiri ya ufukara wa Mtakatifu Klara wa Assisi.
Itakumbukwa
kwamba, kwa mara ya kwanza Monasteri hii ilitembelewa na Papa Paulo wa sita hapo tarehe
3 Septemba 1971, ili kuwashirikisha matunda ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
kuhusu umuhimu wa kufuata Katiba, maisha ya Kijumuiya, Nadhiri na kwamba, kama watawa
walikuwa ni alama ya matumaini ya Kanisa.
Tarehe 14 Agosti 1979, Mwenyeheri
Yohane Paulo II aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Monasteri
hii na kuwaomba Watawa hao kuendelea kusali kwa ajili ya mafao ya binadamu wote na
kwamba, Kanisa linawaangalia kwa jicho la matumaini katika maisha yao yaliyojificha
machoni pa binadamu, lakini Mwenyezi Mungu anasikiliza sala na sadaka yao.
Ilikuwa
ni tarehe 15 Septemba 2007, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipokutana
na kuzungumza na watawa wanaoishi katika Monasteri hii, akiwataka kuwa ni vielelezo
vya moto wa upendo na sala kwa ajili ya kumwombea Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili
aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake aliokabidhiwa na Kristo mwenyewe kwa ajili
ya Kanisa lake.
Aliwakumbusha kwamba, wao ni warithi wa tunu msingi za Kiinjili
na amana iliyoachwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi na Mtakatifu Klara, waliojitoa
kimasomaso kwa ajili ya Mungu na Jirani, wakaishi Nadhiri na wakaonesha heshima ya
kulinda na kutunza mazingira.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliwataka
watawa hao kuonesha ile furaha ya Injili katika hali ya ukawaida pasi na kupenda makuu,
kwa kutambua kwamba, wanatekeleza dhamana na utume wa Kanisa katika ari na mwamko
wa kimissionari. Alisema kwamba, ni matumaini yake kuwa Mwenyezi Mungu ataendelea
kuwaita wasichana wengi na watakatifu wanaotaka kujitoa kwa ajili ya Mungu na jirani
katika maisha ya utawa!