2013-08-14 12:39:08

Kuonyana na kusameheana Kindugu....


Kwa kawaida inachukua miezi au hata miaka kujenga uhusiano wa kirafiki au mahusiano ya kijamii. Hatua ya mwanzo ya kujenga mahusiano ni ile hali ya kutoaminiana. Lakini taratibu na pole pole mmoja anapomwalika mwenzake na kujifunua vile alivyo, hujenga uhusiano madhubuti kiasi ambacho wawili hao waliokuwa tofauti wanaweza kuanza mchakato wakawa ndugu wa damu, au marafiki wa kupika na kupakua.

Na katika mila nyingine za kiafrika hapo zamani, watu waliopendana kwa dhati walichanjiana hata damu zao. Hatua ya juu ya uhusiano huu ni ule alioandika mwandishi John Powell katika kitabu chake - "Kwa nini naogopa kukwambia mimi ni nani" anaiita hatua hii "successful personal Encounter".

Urafiki na undugu ni kitu kitakatifu. Sio kitu cha kidunia. Urafiki ni kushiriki tabia ya kimungu, ambayo kihulka ni upendo wenyewe. Tabia ya upendo wa dhati (unconditional love) ilidhihirishwa na Kristo mwenyewe si kwa maneno tu bali kwa matendo "..mimi nimewaita rafiki kwa vile kila nilichosikia kwa baba yangu nimewaarifuni.."(Yoh 15:14 - 15).

Tofauti na njia ngumu ya kujenga urafiki ambayo uhitaji uvumilivu na kuchukuliana - kuvunja urafiki kunahitaji dakika moja au siku moja tu. Na hatari ya kuvunja urafiki ni kualika ile hali ya wawili kukatiana tamaa na kuona yaliyomwagika hayazoleki tena. Ni kuingia katika uringo wa kuwa na uhasama na chuki ya paka na mbwa.

Leo katika Injili yetu ya Aogosti 14, 2013 ambayo inaambatana na sikukuu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, ambaye alifanya urafiki jela na baba wa familia moja ili asiuwawe - Kristo anataka kusema haya :

1. Kwa vile urafiki na undugu wetu ni tendo la kimungu, na tumeujenga kwa shida na muda mrefu - tujaribu kuutunza urafiki wetu kwa gharama ye yote ile. Hata endapo kibinadamu tukikoseana, kipimo cha msamaha wetu kiwe saba mara sabini (Mt 18:22). Yaani, kila saa na kila dakika tushike sime na ngao ili kuulinda undungu wetu.

2. Kutumia mazungumzo, kujuana mihemuko na mitizamo yetu hualika kupokeana hivyo kuepusha kuingia katika migongano. Mfano baba wa familia ni kigugumizi, mama awe mwangalifu panapotokea kutofautiana aongee kwa upole na utulivu. Mama akiongea kwa haraka na kupayuka humuumiza sana mwenye shida ya kigugumizi. Yaani, tujuane udhaifu na mapungufu yetu.

3. Katika kurejesha uhusiano ulioingia dosari tutumie wenzetu - hasa wazee waliokula chumvi nyingi na wenye busara. Kazi ya wasuluhishi hawa ni kujaribu kutoegemea upande wo wote ili waliogombana watoke wakiwa na mioyo mweupe.

4. Hatua ya kanisa katika kurudisha mapatano hualika kusoma na kusiliza Neno la Mungu, kujongea Sakramenti ya upatanisho na Sala. Anayesamehe ni yule anayesali. Anayesamehe ni yule ashuhudiye mbingu zimefunguka na kuona ya mbinguni kama alivyofanya Mtakatifu Stefano. "..Bwana usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii.."(Matendo 7:59-60).

Tuombe kwa ajili ya familia zetu hasa wana ndoa ambao wameingia katika ugomvi na mafarakano kiasi cha kuvunja ndoa zao. Sala yetu tunaipeleka hasa kwa wahanga wa vita hivi - watoto ndani ya familia, kwa vile wapiganapo Tembo nyasi ndizo ziumiazo.

Cheche za Neno la Mungu kutoka kwa Padre Beno Kikudo, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
All the contents on this site are copyrighted ©.