Chuo Kikuu cha SAUT na mikakati ya kupambana na ujinga Afrika Mashariki
Askofu Bernardin Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa aliyewahi kuwa mkuu wa taaluma
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, katika makala iliyoandikwa
kwenye Gazeti la L'Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican anasema kwamba, Chuo
Kikuu cha SAUT ni kati ya matunda ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linajivunia
katika mikakati yake ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho
na kimwili.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limewekeza kwa kiwango cha
juu katika sekta ya elimu kwa lengo la kutaka kumkomboa mtanzania kutoka katika lindi
la ujinga, maradhi na umaskini. Chuo Kikuu cha SAUT kilichoanzishwa rasmi kunako Mwaka
1998, kimekuwa ni kitovu cha majiundo ya kiakili, kiroho, kimwili na kimaadili kwa
vijana kutoka ndani na nje ya Tanzania. SAUT inapania kuwajengea uwezo wanafunzi wake
ili waweze kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wenzao kwa ari kubwa,
majitoleo, taaluma na uzalendo.
Askofu Mfumbusa anasema kwamba, SAUT katika
kipindi chote hiki imeendelea kujitanua na kwa sasa ni kati ya Vyuo Vikuu Barani Afrika
vyenye idadi kubwa ya wanafunzi. SAUT inaendelea kupokea wanafunzi kutoka Burundi,
Rwanda, Malawi, Uganda, DRC, Kenya, Zambia, Sudan, Ethiopia, Eritrea, Ujerumani na
Finland. Majaalim wake wengi licha ya kuwa ni watanzania, lakini pia kuna mchango
wa Jumuiya ya Kimataifa kutoka katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama vile Benin,
Kenya na Ulaya.
Askofu Mfumbusha anasema, licha ya SAUT kutoa taaluma kwa
kuzingatia viwango vya kimataifa, lakini pia inakazia masuala ya maadili na utu wema,
ili kuwafunda wanafunzi watakaowajibika barabara mbele ya Mwenyezi Mungu na Jamii
inayowazunguka. Rushwa na ufisadi ni kati ya matatizo makubwa yanayoikabili Tanzania.
Kumbe, anasema Askofu Mfumbusa, ikiwa kama vijana hawatapewa misingi bora
ya maadili na utu wema, uzalendo na sadaka; ukweli na uaminifu, wanaweza kujikuta
kwamba, wanatumbukia au kutumbukizwa kwenye dimbwi la rushwa na ufisadi, kwa ajili
ya kupata utajiri wa haraka haraka pasi na jasho.
Kanisa Katoliki nchini Tanzania
linapenda kushiriki kikamilifu katika kuchangia ustawi na maendeleo ya watanzania
wengi, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Bara la Afrika linalopania kujitegemea
na kuwategemeza watu wake kwa hali na mali. Chuo Kikuu cha SAUT kinaendelea kuongeza
vitivo kwa kusoma alama za nyakati na mahitaji ya maendeleo ya sayansi na teknolojia
kwa wakati huu. Chuo kinaendelea kuboresha maktaba zake ambazo ni chemchemi ya ufahamu
na hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali.
Wanafunzi wa Kitivo cha
Mawasiliano ya Jamii wanayo fursa ya kufanya mazoezi kwenye Kituo cha Radio SAUT na
Kituo cha Televisheni kinachoendeshwa na kusimamiwa na wanafunzi wenyewe.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania kutokana na sera makini, moyo wa uzalendo na hali ya
kujitosa kikamilifu bila ya kujibakiza, kunawawezesha kuendelea kutekeleza mikakati
ya kuitanua SAUT ili iweze kuwa karibu zaidi na wanafunzi wake ndani na nje kwa kufungua
Vyuo vishiriki mipakani mwa Tanzania. Askofu Mfumbusa anasema, Chuo Kikuu cha SAUT
ni matunda ya mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.