AMECEA kukutana Lilongwe kuanzia tarehe 16 hadi 26 Julai 2014
Uinjilishaji Mpya kwa njia ya wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani ya Kikristo ndiyo
kauli mbiu itakayoongoza Maadhimisho ya Mkutano wa 18 wa Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, utakaofanyika nchini Malawi, kuanzia
tarehe 16 hadi 26 Julai 2014.
Itakumbukwa kwamba, kunako Mwaka 2011, AMECEA
iliadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa wakati nchi nyingi za Kiafrika
zikiwa katika vuguvugu la kudai uhuru wa bendera. Uimarishaji wa Jumuiya Ndogo ndogo
za Kikristo kama shule ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti, Matendo ya Huruma
na Majiundo makini ya imani, zilipewa msukumo wa pekee na AMECEA katika uhai wake.
AMECEA
imeona na kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinajitokeza miongoni mwa
wananchi wanaounda nchi za AMECEA katika elimu, afya na maendeleo endelevu. Kunako
Mwaka 1976, AMECEA katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji ikaamua kuanzisha
Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA.
Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Agostino cha Tanzania, SAUT ni matunda ya changamoto za Mababa wa AMECEA. Hadi leo
hii, AMECEA inaendelea kucharuka katika masuala ya maisha ya kiroho, elimu, afya na
maendeleo ya Jamii.